NA JOHN BUKUKU – SIMIYU
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bariadi Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Masanja Kadogosa, amewataka vijana kote nchini kuhakikisha wanaitunza amani ya nchi kwa gharama yoyote, akisisitiza kuwa amani haina mbadala.
Akizungumza Oktoba 11, 2025, Kadogosa alisema kuwa jambo la msingi kwa Watanzania, hasa vijana, ni kulinda amani kwani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana pasipo amani.
“Kitu chochote hakiwezi kubadilishwa na amani. Cha kwanza tuzungumze amani iwepo, hata kama kuna kitu unataka, kipatikane kwa njia ya amani. Ukicheza na amani, maana yake unachokitaka hakitatokea,” alisema Kadogosa.
Amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kwa kutotumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa zinazoweza kuvuruga umoja wa kitaifa.
Kadogosa aliongeza kuwa kelele zinazotolewa mitandaoni hazipaswi kuwatoa Watanzania kwenye mstari wa kutunza amani, akirejea maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema kuwa licha ya kelele nyingi, Serikali iliendelea kulinda amani na umoja wa taifa.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameapa kulinda na kuijenga amani, hivyo ni wajibu wa kila kijana na mwananchi kwa ujumla kuhakikisha taifa linabaki salama na lenye utulivu.
Kadogosa pia alibainisha kuwa CCM imeendelea kuimarisha maendeleo katika Kanda ya Ziwa, ambapo miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 440 inaendelea kutekelezwa katika Bariadi, Meatu, Itilima na Maswa.
Aidha, alisema huduma ya umeme inaendelea kusambazwa hadi vitongoji, na sekta ya kilimo pamoja na ufugaji zimeboreshwa kupitia ruzuku ya mbolea na chanjo kwa mifugo, jambo linalowezesha wananchi kuongeza uzalishaji.
Kadogosa alisisitiza kuwa CCM ni chama kinachoamini katika nidhamu na taratibu, na kila mwanachama anatakiwa kufuata misingi hiyo. Aliongeza kuwa hata alipokuwa mtumishi wa umma, aliendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kupitia Mkoa wa Simiyu.
Amesema dhamira yake ya kugombea Ubunge inalenga kushiriki kikamilifu kusimamia utekelezaji wa sera na miradi ya Serikali Bungeni.
“Kazi ya Bunge ni kusimamia yale ambayo Serikali inafanya. Nilikuwa upande mwingine, naamini nitakuwa na uelewa wa kutosha katika kushiriki kutunga sheria na kuhakikisha sera zinatengeneza matokeo chanya kwa wananchi,” alisema Kadogosa.