Na: Dkt. Reubeni Lumbagala
Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa kilimo kimeajiri Watanzania wengi zaidi ya asilimia 60 hasa waishio maeneo ya vijijini. Kutokana na kilimo kuwa na tija, wananchi waishio maeneo ya mjini nao siku hizi wanajishughulisha na kilimo kidogo (small scale agriculture) katika makazi yao hasa kilimo cha mbogamboga na matunda. Kimsingi, kilimo kina tija ukizingatia kinaacha athari chanya ya moja mwa moja hasa katika kuwapatia wananchi chakula na fedha.
Kwa nchi yetu ya Tanzania ambayo tunakubaliana kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu, kama nchi hatuna budi kuweka mikakati madhubuti inayotekelezeka ili kuhakikisha tunakuza kilimo chetu ili kugusa kundi kubwa la wananchi ambao wamejiajiri katika sekta hii. Ikumbukwe kuwa sekta ya kilimo imefungamanishwa pia na sekta za ufugaji na uvuvi.
Umuhimu wa sekta ya kilimo hauishii tu kutupatia chakula na fedha lakini pia kilimo kina mnyororo mkubwa wa thamani. Kupitia kilimo, wafanyabiashara wa usafirishaji wanapata fedha kupitia usafirishaji wa mazao kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Pia, kilimo kinatoa ajira kupitia wafanyabiashara wa mazao ambao wananunua mazao kutoka kwa wakulima na kwenda kuyauza sokoni.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwaka 2021, amefanya makubwa katika sekta ya kilimo hasa katika kuongeza maradufu bajeti ya sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.242 mwaka 2025, ongezeko hili ni sawa na asilimia 322. Ongezeko la bajeti limelenga kutekeleza vipaumbele vya sekta ya kilimo ikiwemo kuimarisha utafiti, matumizi ya zana bora, maendeleo ya umwagiliaji, usalama wa chakula, ushirikishwaji wa kifedha na kuongeza thamani ya bidhaa.
Moja ya mkakati mkubwa unaoweza kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo (agrarian revolution) ni kutoa msukumo mkubwa hasa katika kilimo cha umwagiliaji (Irrigation farming). Hii inatokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu, kilimo chetu kimekuwa kikitegemea mvua na kwa kuzingatia changamoto ya kidunia iliyopo sasa ya mabadiliko ya tabia nchi, maji ya mvua pekee hayataweza kukuza kilimo chetu badala yake tutarudi nyuma kimaendeleo kwani pale kutakapotokea ukame na upungufu wa mvua, kama Taifa tutegemee kuingia kwenye njaa kubwa, kudidimia kwa sekta za viwanda na biashara.
Oktoba 11, 2025, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa katika kampeni za uchaguzi wilayani Maswa mkoani Simiyu alisema atafanikisha ujenzi wa skimu 738 za umwagiliaji nchi nzima ili kukuza zaidi sekta ya kilimo kwa asilimia 10 na hatimaye kuchangia maendeleo ya nchi kwa kasi kubwa.
“Kilimo cha umwagiliaji maji ndicho kipaumbele chetu, tunakwenda kujenga skimu za umwagiliaji 738 Tanzania nzima. Lengo ni kukuza sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2030, nikitoka kwenda kupumzika niache sekta ya kilimo imekuwa kwa asilimia 10 kwa mwaka.” Sambamba na hilo, Dkt. Samia akaongeza kuwa “Sasa hivi tunakua kwa asilimia nne hadi tano, nataka niikuze kwa asilimia 10 kwa mwaka hili ndilo lengo langu. Ninapozungumza sekta ya kilimo ni mifugo na uvuvi vyote vinaingia kwenye kilimo.”
Kimsingi, ujenzi wa skimu 738 za umwagiliaji utaboresha kilimo chetu kutoka kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua hadi kuwa na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji ambapo wakulima wataweza kulima hadi mara tatu kwa mwaka, hali itakayoboresha maisha yao moja kwa moja. Ule wimbo tuliozoea kuusikia ya kuwa “Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu” unakwenda kuimbika vizuri chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ukweli ni kwamba suala la kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzani halitabaki kuwa maneno matupu bali wananchi watajionea kwa macho yao namna kilimo kilivyo na tija kwa kubadilisha hali zao za maisha kwani skimu za umwagiliaji ni kichocheo muhimu cha ukuzaji sekta ya kilimo.
Ni vyema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ijipange vyema kuhakikisha mpango huu wa ujenzi wa skimu 738 unafanikiwa kikamilifu kwani wananchi tunasubiri kwa hamu utekelezaji wake ambao una tija kubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Ni muhimu pia kuzingatia suala la utunzaji mazingira, hii itasaidia kupata maji ya uhakika yatakayotumika katika skimu zetu za umwagiliaji kwa maendeleo ya kilimo na uchumi wetu. Kwa hakika mafanikio ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji ni jambo ambalo litaacha alama kubwa katika historia ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.