Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKURUGENZI wa Glisten Pre & Primary school iliyopo mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Justin Nyari ameisihi jamii kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu wa 2025 ili kuwachagua viongozi bora.
Nyari ameyasema hayo kwenye mahafali ya tano ya wahitimu wa darasa la saba ya shule ya awali na msingi Glisten iliyofanyika shuleni hapo.
Ameeleza kwamba akiwa mwana jamii anakumbusha kuwa Oktoba 29 mwaka 2025 kutafanyika uchaguzi mkuu hivyo watu washiriki zoezi hilo kwa wingi.
“Nikiwa mwana jamii, nawakumbusha kuwa Oktoba 29 mwaka 2025 Taifa letu litafanya uchaguzi, naomba tushiriki kwa amani na utulivu, ili tuendelee kuwa mfano bora kwa watoto wetu katika kulinda mshikamano wa Taifa,” amesema Nyari.
Ameeleza kwamba dunia imeona namna uongozi wa miaka minne wa Rais Samia Suluhu Hassan ulivyokuwa madhubuti na wenye kuwatumikia vyema watanzania.
“Watanzania wameona jitihada za dhati katika kuwatumikia kupitia uongozi wake hivyo ni vyema kujitokeza kwa wingi kumpigia kura na pia mgeni rasmi wetu mgombea ubunge kupitia CCM James Ole Millya,” amesema Nyari.
Hata hivyo, amewaasa wazazi na walezi wa watoto waliohitimu elimu ya msingi kujiandaa vyema kuhakikisha wanafunzi hao wanajiandaa ipasavyo kusoma elimu ya sekondari.
“Mara nyingi wanafunzi wanaohitimu shule hii wanakuwa mabalozi wetu wazuri kwenye taaluma, waliofaulu kwenda sekondari za Ilboru, Tabora boys, Kilakala, Tanzanite tunapata sifa zao wanaongoza huko,” amesema Nyari.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo, James Ole Millya amewasihi wanafunzi hao kuhakikisha wanapambana kuisaka elimu kwani mazingira ya sasa ni rafiki fotauti na miaka iliyopita.
Ole Millya amesema hivi sasa Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi kwenye elimu hivyo wanafunzi watumie fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii ili wake kuitumikia jamii inayowazunguka.
Meneja wa shule hiyo Justice Nyari amewapongeza wahitimu hao kwa kumaliza darasa la saba huku wakijiandaa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2026.
Justice ameeleza kwamba jamii inapaswa kuteketeza kwa vitendo msemo wa aliyekuwa Rais wa Afrika kusini Nelson Mandela kuwa hakuna jamboa muhimu kama elimu.
