Mgombea ubunge Jimbo la Nkasi kaskazini Salum Kazukamwe wakati akizungumza na wanachama na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha mpata
Baadhi ya wananchi na wanachama waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha mpata kata ya Kirando Jimbo la Nkasi Kaskazini.
……………..
Na Neema Mtuka, Nkasi
Rukwa : Mgombea ubunge Jimbo la Nkasi Kaskazini Salum Kazukamwe kupitia chama cha mapinduzi (CCM) amewaomba wananchi wa Nkasi Kaskazini kumchagua ili aweze kuwaletea maendeleo na amewahakikishia kutekeleza ahadi alizowaahidi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya kirando Kijiji cha mpata Kazukamwe amesema anafahamu changamoto zilizopo katika kata hiyo na ameahidi kushughulikia changamoto hizo ili chama hicho kiendelee kukubalika.
“Ninafahamu changamoto zenu kwa upande wa afya ,maji , miundombinu ya barabara pamoja na shule ninawaahidi mkinipa ridhaa nitahakikisha nina punguza baadhi ya changamoto zinazowakabili.”amesema Kazukamwe.
Kazukamwe amesema wataifanya kata ya Kirando kuwa kata ya kimkakati endapo watamchagua yeye kuwa mbunge na madiwani wake ili waweze kuiendesha halmashauri hiyo.
Amesema gharama za kujifungua ni kubwa kwa wakinamama wajawazito wa kata ya Kirando hivyo amewaahidi kuwa atashughulika na changamoto hiyo ili akina mama wajawazito wapate huduma bila usumbufu wowote.
“Mkinichagua mimi kuwa mbunge na kunipa diwani wa kata hii ya Kirando tutashirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo hasa nitaweka msukumo mkubwa ili wavuvi wapate vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki mwambao mwa ziwa Tanganyika.”amesema Kazukamwe.
Mgombea Udiwani kata ya Kirando Kakuli Rashidi Seba amesema yeye sio mzungumzaji nipo kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi naomba kura ili awe mtekelezaji wa miradi mbalimbali katika kata hiyo.
” Nipeni kura ,nichagueni mimi nitawaletea maendeleo na kumalizia pale nilipoishia.”amesema Seba.
Seba amesema tayari ametoa sh mill 5 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho na ameitaka kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo kutoa taarifa ya matumizi katika zahanati ili wananchi wajue pesa inavyotumika.
Aidha amemwombea kura mgombea ubunge ili wakipata ridhaa watashirikiana kwa pamoja katika kupunguza kero za miundombinu ya barabara na mambo mengine ,ni muhimu kupiga kura ili kurudisha Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa chama chao Octoba 29,2025.
Baadhi ya wananchi na wanachama waliojitokeza katika mkutano huo wa kampeni akiwemo Razia Omary amesema uchaguzi wa mwaka huu ni wa kimkakati, hawatakuwa tayari kuzuiliwa kumchagua mtu wanayemtaka.
“ Kwenye swala la ubunge hatuitaji mtu kutuchagulia hivyo tutampigia mgombea wetu Salumu Kazukamwe ambaye anatosha na atatuletea maendeleo katika Jimbo letu.”amesisitiza Omary
Pia amewaomba wagombea ubunge na udiwani kutekeleza ahadi wanazozitoa katika mikutano ya kampeni ili kuweka imani kwa wananchi na wanachama.
Sambamba na hilo pia Omary amemtaka mgombea ubunge kuhakikisha anawasaidia kupata mikopo yenye riba nafuu ili kujikwamua kiuchumi kwani hali ya maisha yao sio nzuri.
” Tunakuomba ukichaguliwa kuwa Mbunge tusaidie kupata mikopo ya riba nafuu,hii mikopo ya kausha damu imetuharibia maisha,ndoa za watu zimevunjika ,na wengine wamekimbia familia zao tunaomba utusaidie.” Amesema omar.