Na John Bukuku – Bukombe, Geita
Wimbi kubwa la wananchi wa Bukombe, mkoani Geita, leo tarehe 12 Oktoba 2025, limejitokeza kwa wingi kushiriki mkutano wa hadhara wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Taswira ya umati mkubwa wa wananchi waliofurika katika viwanja vya mkutano huo ni uthibitisho tosha wa jinsi gani Dkt. Samia amekubalika na wananchi kutokana na kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka minne iliyopita chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Wengi waliokuwa wakishiriki mkutano huo walisikika wakipaza sauti za kumuunga mkono, wakisema wazi kwamba kazi alizofanya Dkt. Samia katika nyanja za maendeleo, uchumi na ustawi wa jamii ndizo zimewaondoa hofu na kuwapa imani kwamba CCM itaendelea kuongoza nchi.
“Dkt. Samia anashindwa aje?” hii ni kauli ambayo imekuwa ikisambaa mitandaoni ikibebwa na wimbo wa mwanamuziki (Harmonize) na picha zinazoonesha mafuriko ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, kama ishara ya mapenzi makubwa ya wananchi kwa mgombea huyo wa CCM.