Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Masanja James akimshauri mwananchi wa Temeke mara baada ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanywa na Hospitali hiyo na kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Jumla ya watu 251 walifanyiwa uchunguzi wa afya.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Ibrahim Amri akimpima kiwango cha sukari kwenye damu mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya ijulikanayo kama Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanywa na Hospitali hiyo na kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Jumla ya watu 251 walifanyiwa uchunguzi wa afya.
Baadhi ya wakazi wa Mbagala wakiwa katika foleni ya kupima shinikizo la damu wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group na kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Jumla ya watu 251 walifanyiwa uchunguzi wa afya.
Daktari wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Joyce Mkodo akimshauri mwananchi wa Mbagala mara baada ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanywa na Hospitali hiyo na kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Jumla ya watu 251 walifanyiwa uchunguzi wa afya. (Picha na JKCI)
……….
Watu 251 kutoka Wilaya ya Temeke kata ya Mbagala na vitongoji vyake wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, ngiri, vidonda sugu, matatizo ya mifupa na mgongo pamoja na tiba ya kinywa na meno.
Matibabu hayo yaliyotolewa na Wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Group yamefanyika katika kambi maalumu ya siku mbili ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba na kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Daudi Wapalila alisema asilimia kubwa ya watu waliofanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo walikutwa na matatizo mbalimbali ya meno.
Dkt. Wapalila alisema baada ya kuwafanyia uchunguzi watu waliojitokeza katika kambi hiyo watu 198 walikutwa na magonjwa mbalimbali hivyo kupewa rufaa kufika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya vipimo zaidi na kuanzishiwa matibabu.
“Watu 38 waliofanyiwa uchunguzi katika kambi hii tumewakuta na matatizo ya shinikizo la damu na sukari, watu 18 walikuwa na shida mbalimbali za mifupa hivyo kuhitaji uchunguzi zaidi, watu 120 walikuwa na shida mbalimbali za meno zilizohitaji uchunguzi zaidi na watu 22 walikuwa na matatizo mbalimbali ya afya yanayohitaji upasuaji”, alisema Dkt. Wapalila
Baadhi ya wananchi waliofanyiwa uchunguzi wa afya katika kambi hiyo waliwashukuru wataalamu kutoka JKCI kwa kuwafikishia huduma za afya bila malipo, kuwapa elimu kuhusu afya bora na kuwahamasisha kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Bakari Mkumba alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la juu la damu hivyo kuudhuria katika hospital binafsi kufuatilia mwenendo wa tatizo hilo lakini baada ya kukutana na wataalamu wabobezi ataanza kufanya kliniki zake za matibabu kwa wataalamu hao.
“Kwakweli nilikuwa siamini kuhusu kambi mbalimbali za matibabu zinazofanywa na wataalamu wa afya kutoka hospitali na vituo vya afya mbalimbali lakini leo baada ya kufika hapa na kukutana na wataalamu wa JKCI nimepata elimu nzuri sana pamoja na dawa za shinikizo la damu, lakini pia nimepewa mbinu za kufuata ili tatizo hili lisisababishe madhara mengine”, alisema Bakari .
Bakari aliomba huduma hizo ziendelee kutolewa mara kwa mara kuwafikia wananchi ili watu wote waweze kupata elimu kama ambayo ameipata yeye kwani itasaidia kupunguza idadi ya watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza.