Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara,Kilimo na Viwanda(TCCIA) Mkoa wa Ruvuma Gideon Mpilime katikati aliyevaa suti,akiwa katika Picha ya pamoja naWafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco)Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa wateja iliyoanza Jumatatu na kumaliza Ijumaa,wa pili kushoto Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Eliseus Mhelela na kushoto Makamu Mwenyekiti wa TCCIA John Haule.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wakigonga Cheers wakati wa kilele cha wiki ya Huduma kwa wateja iliyofanyika katika Ofisi za Shirika hilo mjini Songea
……..
Shirika la umeme Tanzania(Tanesco) Mkoa wa Ruvuma,limefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 551 sawa na asilimia 100 katika Mkoa wa Ruvuma,hivyo kutoa fursa kwa wananchi wa Mkoa huo kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Eliseus Mhelela,wakati akizungumza na wadau na wafanyakazi wa Shirika hilo kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa wateja iliyofanyika katika ofisi ya Tanesco Mjini Songea.
Aidha amesema,jumla ya vitongoji 1,975 kati 3,691 sawa na asilimia 53 vimefikiwa na umeme na kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ili kuhakikisha vitongoji vyote vilivyobaki vinapata umeme kabla ya mwaka 2030.
Amesema,lengo ni kuhakikisha Watanzania wote wanaoishi mjini na vijijini wanafaidika na uwekezaji mkubwa katika nishati ya umeme unaofanywa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Huduma zote tunazotoa kwa wananchi, jambo la kwanza ni umeme,hata tukifanya mambo mengi mazuri lakini kama hakuna umeme ni tutaonekana kama hatujafanya kazi,nawaomba sana wenzetu tuhakikishe umeme unapatikana ili kukuza vipato vya watu,uchumi wa watu,biashara na kubadilisha maisha ya watu na hali zao”alisema Mhelela.
“Serikali imetupa jukumu Tanesco tuwasaidie Watanzania wenzetu wapate umeme wa uhakika ambao utakwenda kubadilisha maisha yao,changamoto zipo lakini tuzitumie kama furs ili zitusaidie kuboresha huduma zetu na wateja wapate huduma bora,kwani tunapotoa huduma bora matokeo yake yataonekana kutokana na watu wengi kupata umeme kwenye maeneo yao”alisema Mhelela.
Amesema,ili kufanikisha mpango huo Serikali imeingia mikataba na wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme katika maeneo mbalimbali ambayo itakwenda kuongeza vipato vya wananchi na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara,Kilimo na Viwanda(TCCIA) Mkoa wa Ruvuma Gideon Mpilime,amewapongeza wafanyakazi wa Tanesco kwa jitihada za uzalishaji,usafirishaji na usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Ruvuma ambao unatajwa uchumi wake kukua kwa kasi.
Amesema,sasa juhudi za Tanesco zimeanza kuonekana kwani wananchi wengi wanaunganishiwa umeme kwa haraka tofauti na miaka ya nyuma ambapo walilazimika kusubiri kwa muda mrefu.
Mpilime amesema kuwa,mshikamano na mipango Madhubuti ya Tanesco ni nguzo muhimu zitakazosaidia kusukuma maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma katika kuwahudumia wateja kwa ufanisi.
Mpilime,amewataka kuendelea kufanya kazi kwa juhudi,maarifa na weledi ili kuhakikisha huduma wanazotoa zinakuwa bora na kufikisha umeme kwenye maeneo ambayo bado hayapata huduma na wananchi wanahitaji kupata umeme kwa ajili ya kufanya shughuli zao za maendeleo.
Katika hatua nyingine,Mpilime amelitaka Shirika la Tanesco kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida na umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia hasa majiko ya umeme.
Mpilime Amesema,matumizi ya nishati safi inasaidia sana kupunguza vifo vya watu hasa akimama na kudhibiti uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
“Suala la matumizi ya nishati safi halina mjadala,kwani ni mkakati na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwahiyo sisi sote ni lazima tuanze na tuendelee kutumia nishafi safi kwenye shughuli zet zinazohitaji umeme kama vile kupika chakula”alisema.
Meneja uhusiano na huduma kwa wateja Allan Njiro amesema,katika wiki ya huduma ya kwa wateja wafanyakazi wa Tanesco Ruvuma wamefanya shughuli mbalimbali ikiwemo kurejesha faida kwa jamii kugawa majiko ya umeme,kutoa zawadi na tuzo kwa wateja wakubwa,vocha za umeme kwa shule na kufunga mita janja kwa wateja.