NA JOHN BUKUKU- KAHAMA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kipaumbele kikuu cha serikali ya awamu ijayo kitakuwa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini, kuhakikisha wanasimama imara na kunufaika na rasilimali za nchi, sambamba na kuvutia uwekezaji wa makampuni makubwa katika sekta hiyo.
Akizungumza Oktoba 11, 2025 katika Viwanja vya Magufuli wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Dkt. Samia alisema serikali itahakikisha wachimbaji wadogo wanapatiwa vifaa vya kisasa vya uchimbaji, ikiwemo mitambo ya uchorongaji na utafiti wa teknolojia ili kubaini aina na ubora wa madini yanayopatikana katika maeneo yao.
Alisema hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuongeza tija na kipato, na hivyo kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa, huku serikali ikiendelea kuvutia wawekezaji wakubwa kwa usawa na uwiano wa manufaa kwa Watanzania wote.
Aidha, Dkt. Samia alisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya madini ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia ajira, biashara ndogondogo, na fursa za uwekezaji zinazochochewa na miradi ya kimkakati kama bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga na reli ya kisasa (SGR) kutoka Tanga hadi Musoma, ambayo itapita katika maeneo ya kanda ya ziwa.
Akizungumzia sekta nyingine, Dkt. Samia alisema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha hospitali, vituo vya afya na zahanati ili huduma za kibingwa zipatikane mkoani Shinyanga bila wananchi kulazimika kusafiri mbali.
Pia aliahidi kuendeleza elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kuendeleza vyuo vya ufundi (VETA), pamoja na shule maalumu kwa watoto wenye mahitaji maalum, lengo likiwa ni kujenga taifa lenye ujuzi na uwezo wa kuchochea maendeleo.
Aidha, alieleza kuwa miradi ya maji safi na salama itaendelezwa kupitia mradi wa TACTIC, unaojumuisha ujenzi wa barabara, mifereji na miundombinu ya mijini, sambamba na ujenzi wa soko la bidhaa za kilimo Sango, kituo cha mabasi Mbulu, na soko la wafanyabiashara wadogo Zongomela.
Aliwataka wananchi wa Shinyanga kuendelea kudumisha amani, kuunga mkono hatua za maendeleo, na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa maendeleo endelevu yanahitaji ushirikiano wa wananchi, wabunge na madiwani katika kutekeleza dira ya taifa lenye uchumi imara.