RAIS Mstaafu Dk.Jakaya Kikwete ameamua kuwatolea uvivu wale ambao wamekuwa wakimzushia kifo ambapo amesema yeye ni mzima wa afya hana mafua wala kichomi na kusisitiza wanaomuombea mabaya watatangulia wao na atahudhuria mazishi yao.
Mzee Kikwete ambaye ni Rais Mstaafu was Serikali ya Awamu ya Nne ameyasema hayo leo Oktoba 10,2025 alipokuwa akiwasalimia wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, katika Mkutano wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulioongozwa na Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
“Wale wanaonizushia kifo kupitia mitandao ya kijamii niwaambie niko salama, afya yangu ni nzuri,sina mafua wala kichomi,wanaomwombea mabaya watatangulia wao na mimi nitahudhuria mazishi yao.”
Kikwete ametoa kauli hiyo baada ya kueleza sababu zinazowafanya wananchi kukiamini Chama Cha Mapinduzi kutokana na mikakati na uwezo wa chama hicho katika kupangilia mambo.
Amesema uwezo huo ndio unasababisha CCM kuendelea kuongoza Serikali, na pale anaposema CCM itaendelea kuongoza nchi, wanainuka watu wengine wasiopenda kauli hiyo na kumzushia kifo.
Pamoja na hayo, Kikwete ametumia fursa hiyo pia kumwombea kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi, na wagombea wengine wa Bagamoyo