Staff Sajenti Ciprian Mhuvi,ambaye pia ni kaimu afisa zimamoto wilaya ya Nkasi wakati akitoa elimu ya kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
Afisa utumishi halmashauri ya wilaya ya Nkasi wakati akizungumza katika mafunzo yaliyotolewa na jeshi la zima moto wilaya.
Baadhi ya watumishi walioshiriki katika mafunzo hayo.
…………….,
Na Neema Mtuka, Nkasi
Rukwa:Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, kupitia jeshi la zima moto na uokoaji leo October 9, 2025, imetoa mafunzo ya kujikinga na majanga ya moto kwa watumishi wa makao makuu wa Halmashauri hiyo wawapo katika mazingira mbalimbali yakiwemo ya kazi.
Aidha lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa watumishi hao juu ya matumizi sahihi ya vyazo vya moto, pamoja na kupunguza na kizuia ajali na vifo vitokanvyo na Moto.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Staff Sajenti Ciprian Mhuvi, ambaye pia ni kaimu Afisa Zima moto wilayani Nkasi, aliainisha visababishi vya moto( vyanzo )katika mazingira mbalimbali kuwa ni uzembe: unaosababishwa na uvutaji holela wa Sigara pamoja na mapishi jikoni, hitilafu ya umeme inayosababishwa na kuzidisha mzigo kwenye vifaa vya umeme ( Extension Cable), kuunga umeme kienyeji, kutokukagua mifumo ya umeme ambapo amebainisha kuwa ni muhimu Kila baada ya miaka mitatu mifumo ya umeme ikaguliwe katika majengo mbalimbali ili kupunguza na kizuia madhara yanayoweza kujitokeza.
Sambamba na hayo Mhuvi aliongeza kuwa, matumizi ya vifaa vya umeme kwa muda mrefu ikiwemo Runinga, Redio, swichi mbovu, uandaaji wa mashamba kwa kuchoma moto na uwindaji ni miongoni mwa vyanzo vya moto vinavyoweza kuleta madhara makubwa katika jamii.
Kupitia mafunzo hayo Staff Sajenti Mhuvi, alisema zipo hatua madhubuti za kuchukua ili kujikinga na moto katika mazingira mbalimbali ikiwemo mahala pa kazi, ambazo ni kutoa elimu kwa umma, kufanya ukaguzi kwenye vyombo vya usafiri na usafirshaji, kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa vya umeme, kuwa na vifaa vya kuzimia moto, mapishi salama pamoja na kuzingatia ujenzi bora hasa kwa kutumia malighafi yenye uwezo wa kizuia Moto kuanzia nusu saa hadi dakika arobaini na tano.
Naye Rainer Mwenda afisa utumishi katika halmashauri hiyo amelishukuru jeshi la zima moto kwa elimu hiyo na wamejifunza namna nzuri ya kutumia baadhi ya vifaa pindi majanga yanapotokea.
Kwa upande wao baadhi ya watumishi waliopatiwa mafunzo hayo akiwemo Valeriani Mwampasi amesema kuwa ni muhimu elimu itokewe mara kwa mara na mafunzo hayo yatawasaidia pindi majanga yanapotokea.