*************
Wananchi katika Soko la Sabasaba mkoani Dodoma jana tarehe 8 Oktoba 2025 walipata nafasi ya kujionea kwa vitendo namna ya kupika kwa umeme kwa gharama nafuu ya chini ya uniti moja yaani chini ya shilingi 350.
Wananchi takribani 100 walitembelea banda la TANESCO mkoa wa Dodoma lililokuwepo katika soko hilo na 70 kati yao walikiri kutumia nishati ambayo si safi na wakaguswa kuhama kuanza kutumia nishati ya umeme kwa kupikia.
“Nimeamini kwamba chakula cha kupika kwa umeme kina ladha ile ile kama cha kupika kwa nishati nyingine na tena ni kitamu zaidi” alisema Bi Mwajabu Fadhili aliyefika kuonja chakula kilichopikwa kwa kutumia majiko janja.
Pamoja na elimu ya nishati safi kwa vitendo, wananchi walipata nafasi pia ya kusikilizwa kero zao mbalimbali zinazowakabili na kupatiwa majibu. Wateja pia walikumbushwa kuhusu kutumia namba 180 ambayo ni bure kwa kutoa taarifa pindi wanapopata changamoto za umeme.