Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera imezindua Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuwatembelea wafanyabiashara na walipa kodi ili kusikiliza changamoto wanazokutana nazo na kuboresha huduma za mamlaka hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Naibu Kamishna wa Upelelezi wa Kodi Tanzania, Ndg. Hashimu Ngoda, alisema lengo ni kuwasikiliza wafanyabiashara na kujua namna wanavyohudumiwa na TRA kwa nia ya kutatua changamoto na kuongeza ufanisi wa huduma.
“Haya yote ni maelekezo ya Kamishna Mkuu kwamba tupite katika maeneo yote ya wafanyabiashara, tuzungumze nao, tuwasikilize ili tujue changamoto zao na namna tunavyowahudumia. Pia tunapokea ushauri kutoka kwao ili kuboresha zaidi huduma zetu,” alisema Ngoda.
Ameongeza kuwa kila mfanyabiashara ana haki ya kupata huduma bora kutoka TRA, na katika Wiki hii ya Huduma kwa Wateja, mamlaka hiyo itawatembelea walipa kodi wote bila kujali kiwango cha kodi wanacholipa.
Ngoda aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa risiti kila wanapouza bidhaa, huku wateja wakisisitizwa kudai risiti na kutumia mashine za EFD, akibainisha kuwa hatua hiyo ni wajibu wa kizalendo unaosaidia katika ukusanyaji wa mapato ya taifa.
Baadhi ya wafanyabiashara waliotembelewa, akiwemo Bi. Husna Mohamed na Kisha Ilamulila, Mkuu wa Shule za Kemebos na Kaizirege, waliipongeza TRA kwa hatua hiyo na kuwasihi wenzao kujitokeza kulipa kodi kwa hiari, wakisema kufanya hivyo ni kuchangia maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.