NA JOHN BUKUKI- BUNDA
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Bunda.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni mjini Bunda, Dkt. Samia alisema kuwa serikali imewekeza katika uvuvi wa kisasa kwa kujenga vizimba 47 vya kufugia samaki, hatua iliyowezesha kuongezeka kwa tija na kipato cha wavuvi.
“Serikali ya CCM imeweka vizimba 47 vya kufugia samaki, na matokeo yake mapato ya wavuvi wilayani Bunda yameongezeka kutoka shilingi bilioni 9.4 hadi bilioni 38.4. Hii imekuwa chachu ya maendeleo kwa familia na uchumi wa wilaya,” alisema Dkt. Samia.
Amesema ongezeko hilo la mapato linatokana na mikakati madhubuti ya serikali katika kusaidia wavuvi wadogo na wa kati, ikiwemo kuwajengea miundombinu ya kisasa, masoko ya uhakika na huduma bora za usafirishaji wa mazao ya uvuvi.
Aidha, Dkt. Samia alisema serikali pia imeboresha barabara ya Nyamuswa–Bulamba yenye urefu wa kilomita 54 pamoja na madaraja kadhaa, ili kurahisisha usafirishaji wa samaki na bidhaa nyingine za uvuvi mwaka mzima bila kuathirika na mvua au jua.
“Tunataka sekta ya uvuvi iwe chanzo cha ajira, lishe na mapato ya uhakika kwa wananchi wetu. Tumeanza vizuri, na tutaendelea kuwekeza zaidi kuhakikisha wavuvi wanapata faida kubwa kutokana na kazi yao,” alisisitiza Dkt. Samia.
Pia, aliwashukuru wananchi wa Bunda kwa mapokezi makubwa, akisema ni ishara ya imani kubwa waliyonayo kwa Chama Cha Mapinduzi na jitihada zake za kuboresha maisha kupitia sekta ya uvuvi.