Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taifa la Tanzania limejiandaa kikamilifu kuwahudumia wananchi wote, wakiwemo vijana na waendesha bodaboda, wanapopata majanga kama vile kuvunjika mifupa au ajali nyingine, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mwendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyarandu alisema Rais Samia ameonyesha uongozi wa kipekee unaoangalia ustawi wa Watanzania wote bila ubaguzi.
Nyarandu alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imefanikiwa kujenga hospitali za wilaya 129 na kukarabati zaidi ya zahanati 1,300, huku idadi ya hospitali zenye uwezo wa kutoa huduma za dharura ikiongezeka kutoka saba (7) mwaka 2000 hadi kufikia hospitali 113 kwa sasa.
“Sio tu kwamba tumeongeza hospitali, bali pia idadi ya wanafunzi wanaohitimu katika fani za sayansi ya afya imeongezeka kutoka 1,800 hadi 3,000 kwa mwaka. Hii ina maana kwamba sasa tuna wataalamu zaidi wanaohudumia Watanzania katika kila kona ya nchi,” alisema Nyarandu.
Aidha, alisema maboresho hayo yameiweka Tanzania katika ramani ya Afrika kama moja ya nchi zenye maendeleo makubwa katika sekta ya afya, jambo lililothibitishwa na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa uwiano wa daktari kwa wagonjwa umeboreshwa kwa kiasi kikubwa.
“Kwa neema ya Mungu na upendo wa Rais Samia, Tanzania sasa ni mfano wa kuigwa barani Afrika. Watu kutoka nchi jirani wanakuja kutibiwa hapa nyumbani kwetu kwa sababu huduma zimeboreshwa na madaktari bingwa wameongezwa,” aliongeza.
Nyarandu alisema hatua hizo ni ushahidi kuwa Rais Samia ni kiongozi mwenye maono ya mbali, hekima na uthubutu katika kuongoza Taifa.
“Dk. Samia amethibitisha kuwa yeye ni kiongozi anayeona mbali. Ameigusa sekta ya afya kwa namna ya kipekee, ameleta matumaini kwa wakulima, wavuvi, wafanyakazi, na vijana wote wanaotegemea huduma bora za tiba,” alisema.
Alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu na huduma za afya, pamoja na kuimarishwa kwa diplomasia na uchumi wa nchi, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kulinda uhai na ustawi wa wananchi wake.