Na Meleka Kulwa -Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, amewataka watumishi wa umma kutumia fursa ya Wiki ya Huduma kwa wateja kama chachu ya mabadiliko ya kiutendaji na kujenga taswira chanya kwa wananchi.
Akizungumza Oktoba 9, 2025, Jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara na waandishi wa habari, Bw. Mkomi amesema kuwa hatua hii itasaidia kupunguza malalamiko, kuongeza tija, na kuendeleza imani ya wananchi kwa Serikali.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa wateja hufanyika kila mwaka kuanzia Oktoba 6 hadi 10, na huhamasisha taasisi za umma kutoa huduma bora na kueleza kwa wananchi huduma wanazozitoa. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “DHAMIRA INAYOWEZEKANA”, inayowataka watumishi kutoa huduma kwa wananchi kwa vitendo.
”Dhamira hii inapaswa kutekelezwa kwa kutumia rasilimali, mipango, na sera sahihi zinazolenga kumsaidia mwananchi, ambaye ndiye mteja wa kwanza wa utumishi wa umma,” amesema Bw. Mkomi.
Amebainisha kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia wajibu na mamlaka waliyopewa kikatiba, kutoa huduma kwa misingi ya uadilifu, na kuzingatia maadili ya taaluma zao. Pia, huduma bora kwa wananchi inahitaji uaminifu, heshima, ukarimu, na kuepuka vitendo vya rushwa” amesema Bw. Mkomi
Bw. Mkomi amebainisha kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kusimamia maadhimisho haya kwa lengo la kuimarisha uzalendo, uadilifu, ubora na utendaji wa watumishi. Maadhimisho pia yanatoa fursa kwa taasisi za umma kujitafakari, kujifunza, na kuboresha taratibu za utoaji huduma kwa wateja.
Aidha, Bw. Mkomi amebainisha umuhimu wa watumishi wa umma kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kwa lengo la kuchagua viongozi wanaofaa katika ngazi ya urais, ubunge, na udiwani kwa maslahi ya taifa.
Aidha, amesema kuwa , watumishi wa umma hawataruhusiwa kwenda kupiga kura nje ya kituo chao cha kazi isipokuwa katika hali maalumu.
Pia, amesema kuwa, Tume ya Uchaguzi inaruhusu mtumishi wa umma ambaye hawezi kupiga kura katika kituo chake cha awali kushiriki katika kura ya Rais pekee.
”Ruhusa hii inatolewa kwa wale walioko safari za kikazi au waliokuwa wamehamishiwa Dodoma baada ya maboresho kufanyika, kuhakikisha haki ya kushiriki uchaguzi wa Rais haipotei kutokana na changamoto za kibinafsi au za kikazi,” amesems Bw. Mkomi.