NA JOHN BUKUKU- MUSOMA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tarime Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Esther Matiko, amesema kuwa kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi wa Jimbo hilo wameahidi kumpa kura za kishindo Oktoba 29 mwaka huu.
Matiko alisema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na kiongozi huyo, ikiwemo fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo katika Jimbo la Tarime kiasi cha Shilingi bilioni 19.7, nje ya miradi ya kimkakati kama vile mradi wa maji wa Tarime–Rorya wenye thamani ya bilioni 134, pamoja na bilioni 9.3 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa katika mji huo.
Matiko ameyasema hayo Oktoba 09, 2025 wakati akizungumza mjini Musoma, kwenye Uwanja wa Karume, katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo alisema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa kiongozi huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema fedha nyingine, mbali na hizo bilioni 19, ni bilioni 3.2 zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Mji wa Tarime, ambapo bilioni 1.7 zilitumika kukarabati jengo la mama na mtoto pamoja na chumba cha kuhifadhi maiti (Mortuary) ya kisasa, sambamba na ujenzi wa jengo la huduma za matibabu na ununuzi wa kichomea taka.
Ameongeza kuwa sambamba na hayo, pia wamekamilisha ujenzi wa nyumba tatu za madaktari, ambazo zimekuwa chachu ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa afya katika mji huo.
Akizungumzia upande wa vifaa tiba, mgombea huyo alisema kuwa kiongozi huyo ameongeza fedha za dawa na vifaa tiba, ambapo mwaka 2020/2021 walitengewa milioni 222, lakini kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wametengewa bilioni 1.2 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.
Matiko alisema kuwa katika mji wa Tarime awali kulikuwa na kituo cha afya kimoja, lakini ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, wamepata kituo cha afya kingine na kuongezewa zahanati, ambazo sasa zimefikia tisa kutoka tatu.
“Tulikuwa na zahanati tatu, lakini katika kipindi cha Rais Dkt. Samia Suluhu tumepata zahanati sita zaidi, hivyo kufikisha tisa zinazotoa huduma za mama na mtoto. Hali hii imepunguza vifo vya mama na mtoto kutoka vifo vitano kwa mwaka hadi kufikia kimoja. Tukimpa miaka mingine mitano, tunaamini hatutakuwa na kifo hata kimoja,” alisema.
Aidha, alisema kuwa amefanikiwa kuongeza idadi ya wahudumu wa afya, ambapo awali walikuwa 176, lakini kipindi cha Rais Dkt. Samia idadi imeongezeka kutoka 103 hadi kufikia 279 ndani ya mji huo.
Katika sekta ya elimu, mgombea huyo alisema kuwa Jimbo la Tarime Mjini limepata bilioni 7.13 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, jambo lililowezesha kuongezeka kwa shule za msingi kutoka 32 hadi 39, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule saba mpya za msingi.
Alisema kutokana na fedha hizo, idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka 14 hadi 22, huku lengo likiwa ni kuongeza madarasa mengi zaidi katika shule za msingi na kuboresha huduma za maji kupitia juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Lakini tumeweza pia kuongeza madarasa ya shule za msingi kutoka 450 hadi 543, na kwa upande wa sekondari tumeongeza kutoka 273 hadi 409. Vyumba vya madarasa vya shule za msingi vimeongezeka kwa 132, na vya sekondari kutoka 156 hadi 276. Madarasa 120 yameongezwa — wana Tarime Mjini tunashukuru, na tunakuahidi Oktoba tutakupigia kura za kishindo kuanzia madiwani, mbunge na wewe Rais Dkt. Samia Suluhu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa katika sekta ya kilimo, wameweza kupata mbolea ya ruzuku zaidi ya tani 600, tofauti na awali ambapo hawakuwa wakipata kabisa. Aidha, vyama vya ushirika vimeboreshwa, jambo lililoongeza tija na manufaa kwa wakulima wa eneo hilo.
Mwisho wa mazungumzo yake, mgombea huyo alimuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 10 ili kuimarisha miundombinu ya mji wa Tarime.