NA JOHN BUKUKU- MUSOMA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wasidanganyike katika kipindi hiki cha kampeni, akisisitiza kuwa maendeleo na maslahi ya wananchi yatatokana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema hayo alipohutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Musoma, akisisitiza kuwa kura kwa wagombea wa CCM ni kura ya maendeleo na mustakabali bora wa Taifa.
“Mnakwenda kupotea mkiwapa wengine, kwa sababu sisi tunakwenda kuweka nguvu zaidi katika huduma za jamii. Mkiwapa wengine wanakwenda kuwafuja na kuwapoteza. Kwa sababu wakiingia kwanza ni kujifunza. Lakini utakapompa jimbo asiyekuwa wa CCM anakwenda kuongea na nani? Atakwenda kumuomba barabara nani? Atakwenda kumuomba maji nani? Kwa sababu serikali ni ya Chama Cha Mapinduzi na yeye ni mpinzani. Ndugu zangu msicheze na hiyo kitu kabisa. Pelekeni kura kwa wateuliwa wa CCM ili safari yetu ya maendeleo iendelee,” amesema Dkt. Samia.
Ameeleza kuwa katika sekta mbalimbali kama maji, umeme, kilimo, barabara, afya na huduma za jamii, Serikali imefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Kuhusu huduma ya umeme, Dkt. Samia amesema Serikali imehakikisha kila kijiji nchini kinafikiwa na umeme, na kwamba kazi inayoendelea sasa ni kusambaza huduma hiyo katika maeneo ya vitongoji.
Amefafanua kuwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM, kuna sera mbili kuu — maendeleo ya jamii na maendeleo ya kiuchumi. Kwa upande wa maendeleo ya jamii, ameeleza kuwa CCM inalenga kuhakikisha wananchi wanapata maji safi, elimu bora, huduma za afya na umeme wa uhakika, mambo ambayo yanachangia kukuza uchumi wa Taifa.
“Tunakwenda kukamilisha maendeleo ya jamii, lakini pia tunaweka nguvu katika maendeleo ya kiuchumi ambayo yanahusisha kilimo, uvuvi, ufugaji na njia za usafiri,” amesema Dkt. Samia.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imejitahidi kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha wakulima kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imetoa mbolea na mbegu kwa ruzuku ili kumwezesha mkulima kuzalisha kwa wingi, hatua ambayo imewezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128.
Kwa mujibu wa Dkt. Samia, ilani ya CCM imeahidi kujenga vituo vya kilimo katika kila mkoa ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo muhimu na kuwawezesha wananchi kunufaika zaidi na jitihada za Serikali katika kukuza uchumi wa Taifa.