NA JOHN BUKUKU- SIMIYU
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Oktoba 09, 2025 anatarajiwa kuunguruma katika mikoa ya Simiyu na Mara, akiendelea na kampeni zake za urais baada ya kumaliza ziara yake katika Kanda ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, Dkt. Samia ataanza mikutano yake ya kampeni katika eneo la Lamadi, kisha ataelekea Busega, na baadaye Bunda, kabla ya kumalizia kwa mkutano mkubwa wa hadhara Musoma Mjini.
Katika mikutano yake, anaendelea kusisitiza uchaguzi wenye amani na utulivu, akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kushiriki kupiga kura bila hofu, akieleza kwamba uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia inayopaswa kufanyika kwa umoja na upendo.
Dkt. Samia amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha hali hiyo inaendelea hata baada ya uchaguzi. Ameongeza kuwa maendeleo hayatawezekana bila amani, ndiyo maana serikali itaendelea kulinda utulivu na usalama wa nchi.
Aidha, anatarajiwa kuwakumbusha wananchi wa mikoa hiyo kuhusu mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa na serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo miradi mikubwa ya barabara, reli, bandari, maji na huduma za kijamii.
Miongoni mwa miradi hiyo ni Daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi), ambalo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafiri na kuokoa maisha ya watu waliokuwa wakipoteza muda mrefu kusubiri vivuko.
Wakazi wa maeneo ya Lamadi, Busega, Bunda na Musoma Mjini wamesema wanasubiri kwa hamu kubwa kumpokea Dkt. Samia, wakieleza kuwa ujio wake ni ishara ya kuthaminiwa kwao na serikali, hasa kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Kanda ya Ziwa.
Wameahidi kujitokeza kwa wingi kumsikiliza na kushiriki uchaguzi kwa amani tarehe 29 Oktoba, wakiahidi kuendelea kuwa mabalozi wa utulivu na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi.