Rufiji, Pwani
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Chumbi–Kiegele yenye urefu wa Kilomita 1.2 kwa kiwango cha lami, ambapo ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Barabara hiyo inajengwa na TARURA wilayani Rufiji mkoani Pwani kwa lengo la kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
“Mkandarasi aliyefanya kazi hii RAPCO CONSTRUCTION amejitahidi kukamilisha kazi kwa wakati, kwa kweli nimeridhika na utekelezaji wa mradi huu, nimuombe Mkandarasi aendelee kufanya kazi kwa ubora na kwa wakati kwenye miradi mingine atakayoweza kuipata ya OR-TAMISEMI kupitia TARURA”, amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana huku akitoa wito kwa Makandarasi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia muda uliopangwa.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema mradi huo umegharimu Shilingi Bilioni 1.499 na utekelezaji wake umefikia asilimia 95, huku ukihusisha uwekaji wa mifereji ya maji ya mvua pamoja na taa za barabarani 18.
“Mkandarasi amejitahidi kufanya kazi vizuri na amekamilisha kwa wakati, tunaamini ni mtanzania mwenzetu ambaye ametuwakilisha vizuri kutekeleza mradi huu ambao utasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi”, amesema.
Wananchi nao wametoa pongezi kwa Serikali kwa kuwaletea maendeleo yanayoonekana kwani hali katika eneo hilo la Chumbi ilikuwa mbaya, walikuwa wanashindwa kusafirisha mazao na mifugo yao lakini ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha usafiri, kukuza biashara na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu kama afya na elimu.