NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniphace Paulo (Nzagamba), ametangaza rasmi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Amesema kuwa amefanya uamuzi huo kwa hiari yake baada ya kutafakari kwa muda mrefu juu ya mustakabali wa siasa na maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo Oktoba 8, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizofanyika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Aidha, amebainisha kuwa hana sababu ya kuendelea kubaki upande wa upinzani ilhali dhamira yake ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.
Amesema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akihudumu kama Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, lakini ameona hakuna haja ya kuendelea kugawanya Watanzania kwa misingi ya itikadi za kisiasa.
Aidha, amebainisha kuwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa wanapaswa kushirikiana katika kuijenga nchi, huku akibainisha kuwa wagombea wote wa ubunge na udiwani katika Mkoa wa Mwanza ni watu wanaofaa na wana uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Amesema kuwa Mwanza ni kitovu cha uchumi wa Kanda ya Ziwa, hivyo kuna umuhimu wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma na kuinua maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa uamuzi wake wa kujiunga na CCM ni sehemu ya kuunga mkono Jeshi la Ukombozi (CCM) linalolenga kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa amani, umoja na mshikamano.
Amesema kuwa hatakuwa tayari kuongoza “jeshi la watu wabaya” na hataki kuwa mnafiki kwa kukaa kimya, bali ameamua kusimama upande wa maendeleo na mabadiliko chanya.
Pia, amesema kuwa anaamini Dkt. Samia ataendelea kuleta mageuzi makubwa nchini, na yeye yuko tayari kushirikiana naye kufanikisha hilo.