NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Baada ya kufanya mikutano mitatu mikubwa ya kampeni katika maeneo ya Buhongwa, Misungwi na Sengerema, Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo (Oktoba 8, 2025) anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni jijini Mwanza, katika Uwanja wa Nyamagana.
Katika mikutano yake ya awali, Dkt. Samia alipokelewa kwa shangwe na maelfu ya wananchi waliomiminika kumsikiliza, ambapo aliendelea kusisitiza umuhimu wa amani, umoja na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Aidha, aliwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika awamu yake ya uongozi, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo iliachwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kama vvile reli ya kisasa (SGR), daraja la Magufuli la Kigongo–Busisi, Miradi mikubwa ya maji Kanda ya ziwa na uboreshaji wa huduma za afya na elimu nchini.
Mkutano wa leo jijini Mwanza unatarajiwa kuvutia maelfu ya wananchi kutoka maeneo yote ya jiji la Mwanza , ambapo viongozi mbalimbali wa CCM wa kitaifa na kikanda wanatarajiwa kushiriki kampeni hizo.
Baada ya mkutano huo Dkt. Samia ataendelea na kampeni zake katika mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, akihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu ili kuendeleza juhudi za maendeleo zilizopo.