NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Chifu Nyamilunda wa Tatu amewahamasisha wananchi wa Ilemela na Nyamagana kushiriki kwa wingi katika kampeni za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa wananchi wanatakiwa kushirikiana kwa umoja na kuunga mkono miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali, huku akitolea mfano wa Chifu Hangaya, Katibu Mkuu Mtendaji wa Machifu Tanzania.
Ameyasema hayo Oktoba 8, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyamagana jijini Mwanza.
Aidha, amebainisha kuwa wananchi hawana haja ya kuwa na wasiwasi, kwani wanaungwa mkono na viongozi wenye weledi na utulivu katika uongozi.
Chifu Nyamilunda wa Tatu amewataka vijana, wazee na akinamama kuungana pamoja katika kampeni za CCM, huku akiwahimiza kutoa kura nyingi na za heshima.
Amesema kuwa shughuli za maendeleo zilizotekelezwa mkoani Mwanza, ikiwemo miradi ya maji ya Butimba na upanuzi wa miundombinu ya Capri Point, zinaendelea kwa kasi, na wananchi wanapaswa kushirikiana kuhakikisha miradi hiyo inawanufaisha wote.
Aidha, amebainisha kuwa miradi ya maji na miundombinu inayojengwa ni ya gharama kubwa na inafaidi jamii kwa ujumla, huku boti na vifaa vya kisasa vikiwasaidia wavuvi kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Chifu Nyamilunda wa Tatu amewaonya vijana dhidi ya kueneza vurugu au maudhui yasiyofaa kwenye mitandao, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya waasisi wa nchi.
Amesema kuwa kampeni zisizo na maadili au zenye mwelekeo wa vurugu haziwezi kuleta maendeleo, bali wananchi wanapaswa kuzingatia utulivu na mshikamano.
Aidha, amebainisha kuwa kushirikiana kama jamii moja na kuunga mkono mgombea wa CCM kutahakikisha ushindi thabiti wa chama na maendeleo endelevu ya mkoa wa Mwanza.