Na WAF, Mpwapwa- Dodoma
Wananchi wa wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma wamejitokeza kwa wingi katika siku za kwanza za kambi ya Madaktari Bingwa na Wabobezi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyoanza rasmi Oktoba 6, 2025, kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa ngazi ya msingi.
Miongoni mwa wananchi waliopatiwa huduma katika kambi hiyo ni Bi Chezelina Gabriel, ambaye amefika hospitalini akiwa na ujauzito wa miezi mitano uliotunga nje ya mfuko wa uzazi ndipo Wataalam wamefanya upasuaji wa dharura ili kuokoa maisha yake.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Dkt. Sophia Kiwango amesema kuwa mgonjwa huyo amepokelewa hospitalini hapo baada ya kuhamishwa kutoka Kituo cha Afya Kibakwe, akiwa na maumivu makali na upungufu mkubwa wa damu.
“Kutokana na hali aliyokuwa nayo, tumeona hakuna sababu ya kusubiri. Mama alikuwa amechoka sana na hali yake ilikuwa mbaya, lakini kwa kuwa hospitali yetu sasa ina vifaa vya kutosha, tumemkimbiza chumba cha upasuaji na kufanikiwa kumuokoa,” amesema Dkt. Kiwango.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Bi. Subira Said, amesema kuwa wananchi wa Mpwapwa na Kongwa wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na makazi yao.
“Niwaombe wananchi tuwe mabalozi kwa wengine. Huduma hizi ambazo Serikali ya Awamu ya Sita imezishusha ngazi za msingi ni matokeo ya maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametambua changamoto za kiuchumi na kuamua kuwasogezea wananchi huduma bora, sambamba na kuwaongezea uwezo wataalam wa maeneo yetu,” amesema Bi. Subira.
Kambi za Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia zimeendelea kufanyika katika wilaya mbalimbali za mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025, zikiwa na lengo la kusogeza huduma za kibingwa ngazi ya msingi na kupunguza rufaa zisizo za lazima.