**********
Serikali, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inatekeleza mradi wa ujenzi wa studio za redio jamii katika Halmashauri mbalimbali nchini. Lengo la mradi huu ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma muhimu za redio, pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika maamuzi ya maendeleo. Pia, mradi unahakikisha habari, burudani, na fursa za maendeleo zinawafikia wote, hususan katika maeneo ya vijijini na yasiyo na huduma za mawasiliano.
Studio hizi za redio jamii zimejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na kuwekwa vifaa vya kisasa vya studio, tayari zinafanya kazi tangu Februari 2024 na zinatoa huduma mbalimbali ikiwemo matangazo ya habari, elimu, burudani, na fursa za maendeleo kwa wananchi.
Kwa njia hii, redio jamii inachangia kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na serikali huku ikihakikisha huduma na fursa muhimu zinawafikia wananchi wote, hasa katika maeneo ya pembezoni.