Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia @wizarahmth , imesaini mkataba wa nyongeza na Kampuni ya Viettel Global Joint Stock, ya Vietnam wenye lengo la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na mtandao wa mawasiliano.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika leo katika Ofisi za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mji wa Serikali Mtumba, ikishuhudiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Adolf Ndunguru, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Majadiliano.
Bw. Ndunguru ameeleza kuwa mkataba huu wa nyongeza unalenga kuimarisha utekelezaji wa makubaliano ya awali kwa kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote, hususan walioko vijijini.
Aidha, amebainisha kuwa nyongeza hiyo pia inashughulikia changamoto zilizojitokeza awali, ikiwemo suala la kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo yaliyo nje ya mkataba bila idhini ya Serikali ya Tanzania.
“Leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni ya Viettel Global. Tunatarajia kuona maboresho makubwa katika sekta ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wote,” alisema Bw. Ndunguru.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Viettel Global Joint Stock, Bi. Nguyen Thi Hoa, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa na imani na kampuni hiyo, na ameahidi kutekeleza kwa ufanisi majukumu yaliyokubaliwa katika mkataba huo.
“Tunaahidi kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Mawasiliano na wadau wengine kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano, bila kujali wapi alipo,” alisema Bi. Hoa.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa awali kati ya Serikali na Kampuni ya Viettel Global ulisainiwa tarehe 16 Julai 2014, ukilenga kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini pamoja na kusambaza huduma za intaneti katika maeneo ya huduma za kijamii ambapo kutokana na changamoto kadhaa za kiutendaji, utekelezaji wa mkataba huo ulisitishwa ili kufanyiwa marekebisho.