*Ujenzi wafikia asilimia 85
*Una viwango vya kutumiwa na Timu zote ikiwemo Simba, Yanga, Azam na nyingine
Chunya
Katika mwendelezo wa kuchangia ukuaji wa sekta nyingine kwa maendeleo ya Taifa na Jamii, shughuli za madini katika Mkoa wa Kimadini Chunya zimechangia ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kisasa Wilayani humo kupitia michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wa Madini chini ya usimamizi ya Halmashauri husika.
Akizungumza katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary kutoka Wizara ya Madini, Mjumbe wa Kamati ya maandalizi ya ujenzi wa uwanja huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa KenGold Sports Club Keneth Mwakyusa amesema kuwa, kujengwa kwa uwanja huo kunatokana na jitihada zilizofanywa na Halmashauri ya Chunya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa Sekta ya Madini zilizowezesha kujengwa kwa uwanja huo wa kisasa wa mpira wa miguu.
‘’ Tunaweza kusema mapato ya madini pia yamehusika katika ujenzi wa uwanja kwasababu wadau waliochangia wapo pia wa madini ambao wametumia fedha zilizotokana na na shughuli za madini lakini wapo na wadau wengine nje ya madini na usimamizi mkuu umefanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chunya akisaidiana na kamati ya ujenzi,’’ amesema.
Ameongeza kwamba, mbali na uwanja huo kutegemewa kutumiwa na timu za Chunya ikiwemo KenGold unatazamiwa katika siku usoni kutumiwa kubwa kama Yanga, Simba, Azam na nyingine huku uwepo wake ukitarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kama hoteli, usafiri, chakula na nyingine na kuongeza kwamba hatua iliyofikiwa hivi sasa ni uwekaji wa nyasi bandia.
Akizungumzia mwenendo wa timu ya Kengold amsema kwamba timu hiyo bado inaendelea na mazoezi na wana Imani kwamba itapanda tena daraja na hivyo kutumia fursa hiyo kuwataka wadau wa michezo nchini wakiwemo wananchi wa Chunya kuendelea kuiunga mkono timu hiyo.
‘’Timu yetu ipo inaendelea na mazoezi, kwa mfano hivi karibuni ilicheza mchezo wa kirafiki na Songwe na zote zilitoka suluhu ya mabao mawili kwa mawili 2-2 kwa hivyo bado tuna imani ya kurejea ligi Kuu,’’ amesisistiza,’’.
Naye, Fundi wa uwanja huo Msafiri Napanja amesema kazi inayoendelea hivi sasa ni uwekaji wa nyasi bandia iliyopangwa kufanyika ndani ya siku 30 huku maendeleo ya ujenzi wa uwanja yamefikia asilimia 85.
Awali, akizungumza na timu hiyo ya Madini Diary, Afisa Madini Mkoa wa Kimadini Chunya Mhandisi Laurent Mayalla amesema kwamba mchango wa Sekta ya madini wilayani chunya umeyagusa maeneo mengi ikiwemo ya michezo kutokana na ujenzi wa uwanja huo.