NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anatarajiwa kuunguruma mkoani Mwanza, akiendelea na kampeni zake za urais baada ya kumaliza ziara yake katika Kanda ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, Dkt. Samia ataanza mikutano yake ya leo katika wilaya ya Misungwi, kisha ataelekea Sengerema, na kumalizia kwa mkutano mkubwa wa hadhara katika eneo la Buhongwa, jijini Mwanza.
Katika mikutano yake, amekuwa akisisitiza Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kushiriki kupiga kura kwa amani, bila kuwa na hofu, akieleza kwamba uchaguzi ni haki ya msingi ya kidemokrasia inayopaswa kutekelezwa kwa utulivu na uzalendo.
Dkt. Samia amekuwa akisisitiza pia umuhimu wa kulinda amani na umoja wa nchi, akisema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa utulivu barani Afrika, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha hali hiyo inaendelea hata baada ya uchaguzi.
Aidha, anatarajiwa kuwakumbusha wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuhusu mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa na serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo miradi mikubwa ya barabara, reli, bandari, maji na huduma za kijamii.
Miongoni mwa miradi hiyo ni Daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi), ambalo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafiri na kuokoa maisha ya watu hasa wagonjwa waliokuwa wakipoteza muda mrefu kusubiri vivuko.