NA JOHN BUKUKU- SENGEREMA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha jina la nchi linabaki na heshima yake ndani na nje ya mipaka, huku akiwataka wananchi kuachana na tabia ya kuisema vibaya Tanzania na badala yake kuitangaza kwa mambo mazuri inayoyafanya.
Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika mjini Sengerema, mkoani Mwanza Oktoba 7, 2025.
Aidha, amebainisha kuwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaheshimika sana duniani kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kukuza uchumi, kuimarisha diplomasia, na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, mifugo na viwanda.
Amesema kuwa baadhi ya Watanzania wamekuwa wakipotosha taswira ya nchi kwa maneno na matendo yasiyo ya kizalendo, jambo linaloweza kudhoofisha heshima ya taifa kimataifa.
“Wapo Watanzania ambao kila wakiona jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaheshimika duniani, kazi yao ni kulishusha. Nawaomba tuachane nao. Waacheni waende kivyao vyao, hao siyo wenzenu,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha sekta zote muhimu zinazochochea uchumi wa nchi, ikiwemo uvuvi, kilimo na mifugo, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zilizopo.
Amesema kupitia sekta ya uvuvi, serikali imejenga vizimba 400 vya kufugia samaki na kuviwezesha viwanda vya kuchakata samaki kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi, ili vijana wazalishe na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa mifugo, Dkt. Samia amesema Tanzania sasa imepata soko kubwa la kuuza mazao ya mifugo nje ya nchi baada ya kuanza kampeni ya kuchanja mifugo kwa ruzuku.
“Tumeleta chanjo za ruzuku, unalipa nusu kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi. Lakini kwa kuku tumesema wote wanachanjwa bure. Lengo ni kuiweka nchi yetu kwenye orodha ya dunia inayotambua nchi zinazochanja mifugo yao,” amesema Dkt. Samia.
Pia, amebainisha kuwa serikali inatekeleza mradi wa utambuzi wa mifugo, ili kuweka rekodi sahihi zitakazosaidia kuongeza uaminifu wa soko la kimataifa na kuinua kipato cha wafugaji.
Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri kwa kujenga barabara, reli, na kuboresha usafiri wa anga na maji, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha uchumi wa viwanda na biashara.
Amesema kuwa katika Ilani ya CCM ya 2025–2030, serikali imepanga kujenga reli tatu kuu—reli ya ukanda wa kusini, reli ya biashara ya kaskazini, na reli ya kati pamoja na kufanyia marekebisho makubwa reli ya TAZARA.
Katika sekta ya anga, amesema kuwa ndani ya miaka mitano iliyopita serikali imeongeza ndege nane, na katika ilani mpya imedhamiria kuongeza nyingine nane ili ATCL iendelee kupanua huduma zake za usafiri wa abiria na mizigo.
Pia, Dkt. Samia amehimiza umuhimu wa ukuaji wa biashara, akitaja mafanikio yaliyopatikana ikiwemo maparachichi na mchele wa Tanzania kuuzwa katika masoko ya Ulaya, jambo linalothibitisha kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi.
Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia viwanda vidogo na vya kati katika kila wilaya, sambamba na kutoa ajira kwa vijana na kuboresha maisha ya wananchi.
“Tunataka kuhakikisha kila Mtanzania yuko karibu na huduma za afya, maji safi, nishati na elimu bora bila kujali hadhi yake ya kiuchumi au kabila, huo ndiyo mwelekeo wa Tanzania mpya yenye maendeleo na heshima duniani,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia amewapongeza wananchi wa Sengerema kwa maendeleo makubwa waliyopata, na kutangaza kuwa wilaya hiyo inatarajia kufungua mgodi mkubwa wa dhahabu, ambao utakuwa mkubwa kuliko yote nchini.
“Huu mgodi utatoa ajira nyingi kwa vijana na biashara nyingi kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Mwanza, niwaombe mjitayarishe vizuri kwa fursa hizo,” amesema Dkt. Samia.