NA JOHN BUKUKU-SENGEREMA
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa somo kwa wananchi jinsi ya kupiga kura kwa usahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Tukio hilo lilitokea mara baada ya Dkt. Samia kuhutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, ambapo alionesha mfano wa namna sahihi ya kupiga kura kwa wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.
Katika maelezo yake, Dkt. Samia amewataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, wakiwa na kadi zao za kupigia kura, na kufuata taratibu zote za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Amesisitiza kuwa ni muhimu kila mpiga kura kuhakikisha anatumbukiza kura yake kwenye sanduku sahihi ili sauti yake ihesabike ipasavyo.
Dkt. Samia ameeleza kuwa kupiga kura ni haki ya msingi ya kila Mtanzania, na ni njia pekee ya kuchagua viongozi wanaostahili kuendelea kuwaletea maendeleo, amani na ustawi wa taifa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutopotoshwa na taarifa za uongo au ushawishi wa watu wanaotaka kuvuruga mchakato wa uchaguzi, akisisitiza kuwa amani na utulivu vinapaswa kudumishwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Amesema kuwa CCM itaendelea kuongoza kwa vitendo kupitia sera na ilani inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania, huku akiwataka wananchi wa Sengerema na maeneo yote nchini kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi bora kwa amani.
“Njooni kwa wingi tarehe 29 Oktoba, mkiwa na kadi zenu za kupiga kura, mchague maendeleo, amani na umoja wa nchi yetu. Kura yako ni sauti yako,” amesema Dkt. Samia.