Na Mwandishi wetu, Mirerani
TIMU ya soka ya Chusa Mining imetwaa ubingwa wa tamasha la Simanjiro Vote & Vibe Festival 2025 kwa kuibwaga Tanzanite veterani kwa bao 1-0 na kujishindia dume la ng’ombe.
Mtanange huo umefanyika katika viwanja vya Tanzanite Complex mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro kwa Mnyalu.
Mashindano hayo yameandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye uchaguzi mkuu kwa kujitokeza kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu wa 2025.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Raphael Lulandala, akizungumza baada ya kukabidhi ng’ombe huyo wa ushindi kwa timu ya Chusa Mining, amewapongeza wachezaji na viongozi kwa ushindi huo.
Amesema kupitia tamasha hilo wametoa elimu hiyo kwa jamii katika kuhakikisha wanashiriki uchaguzi na kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowapenda wao.
“Lengo letu katika tamasha hili ni kuhakikisha watu wanajitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka 2025 kwa ajili ya kupiga kura ya kumchagua Rais, mbunge na madiwani,” amesema DC Lulandala.
Afisa michezo na utamaduni wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Juliana Kiwara amesema michezo hiyo imekuwa kivutio kwa washiriki na mashabiki waliojitokeza kushuhudia burudani mbalimbali.
Kiwara amesema tamasha hilo limeshirikisha timu kutoka Wilaya ya Simanjiro, Wilaya ya Hai na Halmashauri ya Wilaya ya Meru.
Amezitaja timu hizo ni mabingwa wa soka Chusa Mining, washindi wa pili Tanzanite veterani waliopatiwa shilingi 500,000 Kia, Ramasia, watumishi Boma, Meru DC na Alteza.
Mratibu wa tamasha hilo Charles Mnyalu amesema zawadi mbalimbali ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kuku, mipira na fedha taslimu zimetolewa kwa washindi na Mkuu wa Wilaya hiyo Fakii Raphael Lulandala.
“Pamoja na watu kupata ujumbe wa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kujitokeza kupiga kura Oktoba 29 pia wamepata burudani ya michezo mbalimbali.
Mkurugenzi mwenza wa Chusa Mining, Damas Joseph Mwakipesile, amewapongeza vijana wake kwa kushinda mchezo huo wa soka na kumchukua ng’ombe.
Damas amesema vijana wake wameonyesha kandanda safi na kuwa mabingwa wa soka wa Simanjiro Vote & Vibe Festival kwa mwaka huu wa 2025.
Katika tamasha la Simanjiro vote & vibe Festival limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa pete, wavu, kufukuza kuku, drafti, rede, kukuna nazi na kunywa soda na mkate.