NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Mgombea ubunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, amempongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini, hususan sekta ya maji.
Akizungumza kwenye mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika kwenye uwanja wa Tabasam Mjini Sengerema, Mkoa wa Mwanza Oktoba 7, 2025, Aweso amesema kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika miradi ya maji kutokana na uongozi wa Dkt.Samia.
Amesema kuwa Tanzania imekuwa kinara barani Afrika katika utekelezaji wa miradi ya maji na imepokea tuzo mbili — moja iliyotolewa Mlimani City, Dar es Salaam na nyingine nchini Afrika Kusini, ikiwa ni ishara ya kutambuliwa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Aidha, Aweso amebainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya matendo mema ya Dkt. Samia kwa Watanzania, akisisitiza kuwa mioyo ya binadamu huonyesha upendo kwa mtu anayewatendea mema.
Amesema kuwa Dkt. Samia amefanya kazi kubwa katika muda mfupi, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, afya na huduma nyingine za kijamii, na hivyo Watanzania wana wajibu wa kumshukuru na kumuombea aendelee na kazi hiyo.
“Jukumu tulilonalo ni kumuombea kiongozi wetu arudi kwa kishindo ili akamilishe kazi aliyoianza, kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema Aweso.
Aidha, Aweso amebainisha kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, na njia pekee ya kupata viongozi bora ni kupitia uchaguzi, akisisitiza kuwa uchaguzi si mchezo wa bahati nasibu bali ni maisha.
Amesema kuwa yapo mataifa ambayo viongozi wake hawana uzoefu wa kutatua matatizo ya wananchi, lakini Dkt. Samia amethibitisha uwezo wake kupitia utekelezaji wa kazi zinazogusa maisha ya Watanzania moja kwa moja.
Aweso ametoa wito kwa Watanzania kuungana na kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia na Chama Cha Mapinduzi ili kuendeleza amani, umoja na maendeleo nchini.
“Amani ya Tanzania tutaipata chini ya Chama Cha Mapinduzi, na maendeleo yanaonekana kupitia jitihada za Rais wetu. Tumuombee aendelee ili amalizie kazi kubwa aliyoianza,” amesema Aweso.
Aweso amewakumbusha wananchi wa Sengerema na Buchosa kuwa tarehe 29 Oktoba 2025 ni siku muhimu ya kuchukua hatua ya kumchagua Dkt. Samia ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu hii ya uongozi.