Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ufalme wa Uholanzi Mheshimiwa Marjo Johanna Jacoba Crompvoets, katika hafla iliyofanyika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Kombo amempongeza Mheshimiwa Crompvoets kwa uteuzi wake na amemuhakikishia ushirikiano wakati wote atakapokuwa anahudumu hapa nchini.
Aidha Waziri Kombo ameipongeza Serikali ya Uholanzi kwa jitihada za kuanzisha miradi mbalimbali inayoigusa jamii moja kwa moja na kuleta maendeleo ya jamii ikiwemo katika sekta za miundombinu, elimu, afya, mifugo, biashara na uwekezaji na utalii.
Naye Mhe. Crompvoets ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano uliopo na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kupitia maeneo ya kipaumbele yakiwemo kilimo cha mbogamboga, matunda na maua.