Na John Bukuku, Dar es Salaam
Kampuni ya TTCL Corporation imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, ikiahidi kuendelea kuboresha huduma zake za mawasiliano na kuwa karibu zaidi na wateja wake kote nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, alisema wiki hiyo ni fursa muhimu kwa watumishi wa TTCL kujitathmini na kukumbuka wajibu wao wa msingi wa kumweka mteja mbele kama kiini cha mafanikio ya shirika hilo.
“Wiki hii ni kipindi cha kujitathmini, kusikiliza wateja wetu kwa makini, na kuimarisha uhusiano wa kudumu nao. Kaulimbiu ya mwaka huu, ‘Mission: Possible,’ inatukumbusha kwamba hakuna lisilowezekana tukiamua, tukibuni, na tukishirikiana,” alisema Bi. Moshi.
Aliongeza kuwa TTCL imejipanga kuhakikisha huduma bora, nafuu na zenye ubora wa kimataifa zinawafikia Watanzania wote kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu na teknolojia za kisasa.
“Kupitia Mpango Mkakati wa TTCL, tumejikita katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuleta huduma bunifu na za kisasa. Tunalenga kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa heshima, haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu,” alisisitiza.
Bi. Moshi alisema shirika linaendelea kupanua Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikia wilaya zote nchini, sambamba na ujenzi wa minara 1,400 ya mawasiliano vijijini, hatua itakayowawezesha wananchi kupata huduma bila vikwazo.
Aidha, alisema kupitia huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako,” TTCL inaendelea kuhakikisha huduma ya intaneti ya kasi, ya uhakika na yenye viwango vya kimataifa inawafikia Watanzania mijini na vijijini.
“Tunatambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja wetu, na ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na mifumo ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora popote alipo,” alisema Bi. Moshi.
Pia aliwahimiza wateja wa TTCL kuendelea kutumia Kituo cha Huduma kwa Wateja cha saa 24, pamoja na mitandao ya kijamii na maduka ya TTCL kwa ajili ya kupata taarifa, ushauri na huduma mbalimbali.
Uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025 kwa upande wa TTCL umebeba ujumbe wa kuimarisha ubunifu, ushirikiano na dhamira ya kuwahudumia Watanzania kwa viwango vya kimataifa, sambamba na kulifanya shirika hilo kuwa nguzo ya mawasiliano bora Afrika Mashariki na Kati.