Yahusishwa na Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika 2025
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua rasmi Kituo kipya cha Huduma cha TotalEnergies Kimara, ikiwa ni kituo cha kwanza cha kampuni hiyo katika eneo hilo, hatua inayolenga kuwakaribia zaidi wateja wake kwa kuwapatia mafuta ya ubora wa juu na huduma bora, rahisi na za kuaminika.
Uzinduzi huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika 2025, ambayo mwaka huu inabeba kaulimbiu isemayo “Imani Yako, Nguvu Yetu Kila Siku.”
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Marketing Tanzania, Bwana Mamadou Ngom, alisema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kupeleka huduma za nishati karibu zaidi na wananchi.
“Tunapozindua rasmi Kituo cha Huduma cha Kimara, tunaanza pia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika. Hii ni wiki maalum ya kuthamini wateja wetu na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati yetu. Mafanikio ya TotalEnergies yanatokana na imani ambayo wateja wetu wanaendelea kutuonyesha kila siku,” alisema Ngom.
Aidha, alisema kituo hicho kipya kitatoa huduma mbalimbali zikiwemo mafuta ya Excellium, huduma za kadi za mafuta (Fuel Card Services), mafuta lainishi ya ubora wa juu, pamoja na gesi ya kupikia ya TotalEnergies, vyote vikiwa chini ya mpango wa Dealer-Owned-Dealer-Operated (DODO) unaowezesha upanuzi wa mtandao wa kampuni hiyo nchini kote.
“Kituo cha Kimara ni alama ya uaminifu, ushirikiano na maendeleo — tunalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za nishati zenye ubora wa hali ya juu na salama kwa matumizi ya kila siku,” aliongeza Ngom.
Kwa upande wake, mmiliki wa kituo hicho, Bwana Godfrey Nyashage, alisema uamuzi wake wa kushirikiana na TotalEnergies umetokana na imani yake kwa chapa hiyo na misingi imara inayosimamia.
“Nilichagua TotalEnergies kwa sababu naamini katika nguvu ya chapa yao na maadili yao ya uaminifu. Tangu mwanzo walinipa ushirikiano mkubwa na kuniwezesha kujenga kituo hiki cha kisasa. Ushirikiano huu si wa kibiashara pekee, bali ni wa kiimani, na leo umezaa matunda kwa kuzindua kituo cha kwanza cha TotalEnergies hapa Kimara,” alisema Nyashage.
Uzinduzi wa Kituo cha Huduma cha TotalEnergies Kimara unaashiria hatua muhimu katika mkakati wa kampuni hiyo wa kuendelea kupanua huduma zake nchini Tanzania. Kupitia ubunifu, ushirikiano wa kuaminika na mtazamo unaomlenga mteja, TotalEnergies inaendelea kutoa suluhisho za kisasa, salama na bora za nishati zinazokidhi mahitaji ya kila siku ya Watanzania.