Na Meleka Kulwa – Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Ushirika, Kinyaki Obi Kinyaki, amesema kuwa benki hiyo ipo kwa ajili ya kuipatia jamii nzima, wateja na wafanyakazi huduma bora za kifedha kupitia matawi yake nchini.
Ameyasema hayo Oktoba 6, 2025 katika Uzinduzi wa wiki ya huduma kwa Wateja, iliyofanyika Jijini Dodoma katika Viwanja vya Benki hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa benki hiyo kwa sasa ina matawi manne yanayojitegemea ambayo ni Dodoma (Makao Makuu), Tabora, Tandahimba na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Pia, Kinyaki amesema kuwa Benki ya Ushirika inaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Songwe, Manyara na Lindi kupitia njia za kidigitali, huku ikiendelea na maandalizi ya kufungua matawi mengine Mtwara, Kagera, Mbeya na Mwanza.
Aidha, amesema kuwa Benki ya Ushirika ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Aprili mwaka huu, ikiwa na dhamira ya kutoa huduma za kifedha kwa Watanzania na hata wageni wasio raia wa Tanzania.
Pia, Kinyaki amesema kuwa katika Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya Ushirika imejipanga kutoa huduma bora kwa wafanyakazi na jamii kwa ujumla, ikiwemo kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi katika taasisi za kifedha ili kuboresha huduma zaidi.
Amebainisha kuwa tangu kuanza kwa shughuli zake, benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 49 hadi 50, huku amana zilizokusanywa zikifikia zaidi ya bilioni 50.
Aidha, amebainisha kuwa vitabu vya kifedha vya benki hiyo vinaonyesha thamani ya zaidi ya bilioni 98, ishara kuwa jamii imepokea vizuri huduma zinazotolewa na Benki ya Ushirika.
Pia, amesema dhamira kubwa ya benki hiyo ni kusaidia Serikali katika kuleta ujumuishi wa kifedha, ambapo asilimia 51 ya wamiliki wa hisa ni vyama vya ushirika ambavyo pia ni wateja wa benki hiyo.
Aidha, Kinyaki amebainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma bora za kifedha, kupitia mifumo ya kisasa kama huduma za simu, mtandao na mawakala.
Pia, amesema kuwa benki hiyo ina huduma za kadi za Visa zinazowawezesha wateja kutoa pesa katika ATM au kupitia mawakala waliopo nchi nzima, jambo linaloonyesha urahisi wa kupata huduma bila kulazimika kufika makao makuu ya benki hiyo.
Kinyaki amesema kuwa Benki ya Ushirika ni benki ya kidigitali iliyozaliwa katika ulimwengu wa kidigitali, na itaendelea kuboresha mifumo yake ya kiteknolojia ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, haraka na salama.
Aidha, amewakaribisha wananchi wote kujiunga na Benki ya Ushirika, akibainisha kuwa benki hiyo imekuja kuleta ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wote bila ubaguzi.
Kwa upande wake mmoja wa wateja wa benki hiyo, Justin Mogendi, amesema kuwa Benki ya Ushirika imekuwa mkombozi mkubwa kwa Watanzania, hususan wakulima wa vijijini na mijini kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Aidha, amesema kuwa tofauti na benki nyingine, Benki ya Ushirika ina masharti rafiki kwa wakulima, wajasiriamali na wanachama wa vyama vya ushirika, kwani wanashiriki moja kwa moja kama wamiliki na wateja wa benki hiyo.
Pia, Mogendi amebainisha kuwa benki hiyo inatoa mikopo bila urasimu mkubwa, na baadhi ya wanachama hutumia hisa zao kama dhamana ya kupata mikopo, jambo linalowarahisishia wakulima kupata mtaji wa kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Aidha, amesema kuwa huduma za benki hiyo ni za kisasa na kidigitali, ambapo mteja anaweza kutoa fedha kupitia benki yoyote nchini kwa kutumia kadi ya Visa, bila kujali kama eneo husika lina tawi la benki hiyo au la.
Pia, Mogendi amesema kuwa anaamini Benki ya Ushirika itakuwa miongoni mwa benki bora zaidi nchini katika siku zijazo kutokana na ubunifu, huduma bora na mchango wake katika kukuza sekta ya kifedha nchini.
Aidha kwa upande wake, Amina Adamu Ibengwe, mjasiriamali na mnufaika wa huduma za benki hiyo, amebainisha kuwa tangu kuanza kwa benki hiyo wamekuwa wakipata huduma bora na mikopo rahisi kupitia vikundi vya wajasiriamali, jambo lililowawezesha kupiga hatua kubwa katika biashara zao.