Rvuma, Tunduru
Msafara wa mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, umewasili katika wilaya ya Tunduru, mkoa wa Ruvuma, ambapo umefanya mkutano mkubwa wa kampeni.
Akihutubia wananchi wa Tunduru mjini katika viwanja vya Amazon na wananchi wa kijiji cha Nyakapanya, Mhe. Doyo aliwaahidi wananchi hao kuwa endapo watampa dhamana na ridhaa ya kuwa urais, atahakikisha anarejesha kiwanda cha kubagua korosho cha Wilaya ya Tunduru. Amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa nguzo muhimu ya kuinua uchumi wa wananchi wa Tunduru na kuchochea maendeleo ya mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Mhe. Doyo amesema kuwa utekelezaji wa mpango huo wa kufufua kiwanda ambacho thamani yake haizidi shilingi bilioni mbili, umekuwa ukikwamishwa na uzembe na dharau za viongozi wa chama tawala (CCM) kwa wananchi wa Tunduru. “Kama ukiangalia idadi ya mabango ya CCM, na kila bango moja lina thamani ya takribani shilingi elfu ishirini, utagundua kuwa tatizo si ukosefu wa fedha bali ni uzoefu wa kufanya mambo kwa mazoea. Miaka 60 ya utawala wao imekuwa ya kurudia makosa yale yale,” alisema Mhe. Doyo.
Aidha, Mhe. Doyo amewaahidi wananchi kuwa endapo watamchagua, kufufuliwa kwa kiwanda hicho kutachukua si zaidi ya siku 10, kwani tayari wapo wawekezaji walioonesha nia ya dhati ya kuwekeza. Ameongeza kuwa changamoto zilizokwamisha uwekezaji huo ni matokeo ya urasimu, ambao katika utawala wake utakomeshwa mara moja.
“Kiwanda hiki kitakuwa chanzo kikuu cha uchumi wetu. Haiwezekani fikra za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, za kuanzisha viwanda vya kuchakata korosho zipotee hivi hivi. Nichagueni, muone mabadiliko ya kweli,” alisisitiza Mhe. Doyo.
Akiendelea, Mhe. Doyo aliahidi kuwa serikali yake itawakopesha wananchi mashine ndogo za kubangua korosho ili kuongeza thamani ya mazao yao. Amesema hatua hiyo itasaidia wakulima kuuza korosho kwa hadi shilingi elfu ishirini (20,000) kwa kilo badala ya shilingi elfu mbili (2,000) wanazopata sasa. Amewaomba wananchi wa Tunduru na Ruvuma kwa ujumla kumfanyia kampeni za nyumba kwa nyumba, ili mabadiliko ya kiuchumi yaanze katika maisha ya mtu mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Kina Mama Taifa, Bi. Zaidat Fundi Majiamoto, amewataka kina mama wa Tunduru kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Mhe. Doyo na Chama cha NLD, kwa kuwa chama hicho kinajali maslahi ya wananchi. Amesema changamoto kama kutembea umbali mrefu kutafuta maji, au kukosa vifaa vya uzazi hospitalini, ni ishara ya kudhalilisha utu wa mwanamke na si taswira nzuri katika jamii yetu. “Tumpigie kura Mhe. Doyo ili aondoe fedheha hizi na kuleta heshima kwa wanawake wa Tanzania,” alisema Bi. Majiamoto.
Naye Mhamasishaji Mkuu wa kampeni, Bi. Adija Dikulumbale, amesema kuwa wazee wa Ruvuma waliowahi kupigania uhuru wamesahauliwa, kwani maendeleo katika mkoa huo yamekwama kwa muda mrefu. “Huu ni muda wa mabadiliko. Mchagueni Doyo Hassan Doyo muone tofauti. Ameahidi kuleta mwekezaji ndani ya siku 10 na kuondoa urasimu unaokwamisha juhudi za kurejesha viwanda. Hii itazalisha ajira nyingi na kuongeza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja,” alisema Bi. Dikulumbale.
Msafara wa kampeni za Mhe. Doyo Hassan Doyo kupitia Chama cha NLD unaelekea katika wilaya Kirwa, Rufiji, Kibiti, Dar es Salaam na Morogoro.