Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuurejesha Mji wa Chake Chake katika hadhi yake ya kihistoria na kuufanya kuwa kitovu cha biashara na ajira kwa wananchi wa Pemba.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Chanjaani, Jimbo la Chake Chake, Othman alisema serikali atakayoiongoza itatekeleza mipango ya kuinua uchumi wa Pemba kwa kuimarisha miundombinu, biashara na huduma za kijamii.
Alisema Chake Chake na miji mingine kama Wete, Mkoani na Micheweni itapewa kipaumbele katika maendeleo ya miji, ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya biashara na ajira kwa vijana.
Othman alibainisha kuwa Pemba ina fursa nyingi za maendeleo ambazo zitapewa nguvu mpya kupitia sekta za uvuvi, utalii na kilimo, ambazo zina uwezo mkubwa wa kuinua kipato cha wananchi.
Aliahidi pia kuweka mazingira bora ya biashara kwa kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, sambamba na kukuza uwekezaji utakaonufaisha wakazi wa visiwa hivyo.
Aidha, alisema serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha kila Mzanzibari anapata nafasi sawa ya kustawi kiuchumi bila kulazimika kuhama kutokana na ugumu wa maisha.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walieleza kuridhishwa na sera za mgombea huyo, wakisema zinaonesha mwelekeo wa maendeleo na matumaini mapya kwa wananchi wa Pemba, hususan vijana na wanawake wafanyabiashara wadogo.