MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman (OMO), ameahidi kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vya Zanzibar, akisisitiza kwamba Serikali yake itahakikisha kila Mzanzibari anahisi kuwa sehemu ya nchi bila kujali umbali alipo.
Othman ameyasema hayo mara baada ya kuwasili Kisiwa cha Fundo, kilichopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, eneo lililopo umbali wa takribani kilomita 10 kutoka bandari ya Wete, safari inayochukua takribani dakika 30 kwa mashua ndogo kupitia Bahari ya Hindi.
Kisiwa hicho, chenye wakazi wapatao watu 1,200, kimekuwa miongoni mwa maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Othman amesema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuvithamini visiwa vidogo licha ya mchango mkubwa wanaoutoa kupitia sekta ya uvuvi.
Amesisitiza kuwa katika Serikali atakayoiongoza yeye, atahakikisha wananchi wote wanaoishi kwenye visiwa wanapata huduma stahiki kama ilivyo kwa wananchi wanaoishi mijini.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali yake itaweka mifumo bora ya kuimarisha sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia wavuvi boti za kisasa zitakazowawezesha kufika katika kina kirefu cha bahari kwa usalama zaidi, sambamba na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi na kusindika samaki.
Aliahidi pia kuboresha huduma za afya, hasa huduma za uzazi kwa wajawazito, ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Fundo na visiwa jirani. Alisema kuwa ni aibu kuona mama wajawazito wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za haraka, hivyo Serikali yake itahakikisha zahanati za kisasa zinajengwa katika kila kisiwa, zikiwa na madaktari na vifaa vya kisasa.
Katika sekta ya elimu, Othman amesema ataunda mifumo ya elimu inayozingatia mazingira ya bahari na uvuvi ili kuwapa vijana wa visiwani ujuzi wa kujiajiri na kuchochea uchumi wa maeneo yao.