* Awataka wananchi kujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 29, 2025
NA JOHN BUKUKU-BABATI MANYARA
Babati. Mbunge wa zamani wa Simanjiro, Christopher Olesendeka, amewataka wananchi wa Mkoa wa Manyara kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kupiga kura Oktoba 29, ili kumchagua Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Babati, Olesendeka alisema kuwa Dkt. Samia amekuwa kiongozi wa kipekee aliyegusa maisha ya makundi yote ya kijamii – wakiwemo wakulima, wavuvi, wachimbaji wa madini na wafugaji – ambao ndio kundi kubwa linaloishi katika mkoa huo.
“Serikali ya Dkt. Samia imebeba mzigo mkubwa wa kuwawezesha Watanzania, hasa kupitia elimu bure kuanzia shule za awali hadi sekondari, pamoja na mikopo mikubwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” alisema Olesendeka.
Aliongeza kuwa mafanikio haya yanatokana na uimara wa CCM kama chama tawala, akirejea kauli maarufu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema:
“Chama madhubuti huzaa serikali madhubuti; chama legelege huzaa serikali legelege.”
Kwa mujibu wa Olesendeka, misingi ya haki, utu na usawa iliyojengwa na CCM imeendelea kutafsiriwa vizuri kupitia mipango ya maendeleo ya kila mwaka hadi miaka mitano, sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
“Ilani ya CCM ya mwaka huu ni nyenzo muhimu katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa. Dkt. Samia ni kiongozi mbunifu na mzalendo ambaye ameendeleza uhuru wa nchi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa,” aliongeza.
Aidha, alizungumzia mabadiliko yaliyofanywa ndani ya chama hicho katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, akieleza kuwa uteuzi wa vijana wengi ni uthibitisho kuwa CCM ni chama chenye sura ya jamii nzima.
“Hata sisi wazee tuliopisha nafasi hatuna kinyongo. CCM ni kama timu ya mpira – leo unapanga wachezaji hawa, kesho wengine. Haya ni mambo ya kawaida katika chama cha kisiasa,” alisema.
Akimalizia hotuba yake, Olesendeka alisema kuwa CCM imeendelea kuwa mtetezi wa wakulima na wafanyakazi, na kwamba ushindi wa chama hicho ndiyo njia pekee ya kuhakikisha matarajio ya Watanzania kutoka makundi yote ya kijamii yanatimia