Na,Sophia Kingimali.
Mgombea mwenza wa chama cha NCCR-Mageuzi, Everine Munisi, amewaomba wananchi wa jimbo la Kibamba na maeneo jirani kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura ili kuleta mageuzi wanayoyatarajia.
Akizungumza leo octoba 4,2025 Mbezi jijini Dar es salaam kwenye mkutano wa kampeni Munisi amesema yeye ni mkazi wa eneo hilo na anafahamu vyema changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo atahakikisha changamoto hizo zinapatiwa suluhisho endapo watapewa ridhaa ya kuongoza.
Munisi ameeleza kuwa moja ya kero kubwa ni mazingira yasiyo rafiki kwa wafanyabiashara wadogo hivyo Ameahidi kuwa serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayeondolewa kiholela katika eneo lake la kujipatia kipato. “Tunataka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, kwani ndiko maisha ya wananchi wengi yanapojengwa,” amesema.
Aidha, mgombea huyo amewaasa wananchi kuchagua viongozi wanaofaa badala ya viongozi wanaopendwa kwa urafiki au upendeleo kwani viongozi sahihi ndio watakaosaidia taifa kupiga hatua za maendeleo. “Msichague kwa mapenzi, chagueni kwa uwezo na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi,” ameongeza Munisi.
Munisi pia amebainisha kuwa chama cha NCCR-Mageuzi kimejipanga kusimama na vijana kwa kuhakikisha hawabaki nyuma katika harakati za kujenga uchumi wa taifa. Alisema hakuna uwekezaji wowote utakaofanyika bila sauti ya vijana, kwani rasilimali zilizopo nchini lazima wanufaike kwanza wazawa.
Akizungumzia sekta ya madini na utalii, Munisi amesema taifa lina utajiri mkubwa wa rasilimali lakini vijana bado wanalalamikia ukosefu wa ajira hivyo ameahidi kuwa serikali ya NCCR-Mageuzi itasimamia usawa kwa kuhakikisha wazawa ndio wanufaika wa kwanza wa rasilimali hizo. “Hatutaruhusu wageni waje wanufaike wakati Watanzania wapo,” amesema.
Alizungumzia wanawake na makundi maalum, Munisi alisema chama hicho kitaweka mfumo wa uwezeshaji kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuhakikisha kila kundi linapata fursa ya kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi. “Tutapunguza masharti magumu na kuhakikisha kila mwanamke na kila kijana anawezeshwa,” aliongeza.
Katika sekta ya afya, mgombea huyo amesema licha ya kuwepo kwa hospitali, bado kuna uhaba mkubwa wa vifaa tiba na watoa huduma hivyo ameahidi kuboresha huduma hizo na kuhakikisha wagonjwa hawalazimiki kulala wawili katika kitanda kimoja, pamoja na kuwezesha wananchi wasiokuwa na uwezo kupata matibabu.
Munisi amewataka wananchi kulinda amani ya taifa, akiwatahadharisha dhidi ya watu wanaotumia siasa za uchochezi kujaribu kuharibu mshikamano wa kitaifa Amesema NCCR-Mageuzi
imejipanga kuanzisha mijadala ya amani itakayoshirikisha vijana ili kuimarisha mshikano na kudumisha umoja wa taifa.
Pia alisisitiza kuwa chama hicho kitaweka utaratibu mzuri wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuwasaidia kujifunza nidhamu, maadili na ukakamavu, ikiwa ni sehemu ya kujenga kizazi kinachowajibika kwa taifa.
Kwa upande wa miundombinu na huduma za kijamii, Munisi amesema wanatarajia kuona mageuzi makubwa katika sekta ya maji safi na salama, barabara na pia mazingira ya kazi kwa wauguzi huku Aliahidi kuwa mishahara ya wauguzi itakuwa ikipandishwa kila mwaka ili kuondoa vitendo vya rushwa na kuimarisha nidhamu kazini.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Kibamba, Lightiness Laizer, amesema ndani ya miaka saba amekuwa akihudumia jamii katika nyanja mbalimbali, na endapo atapewa ridhaa ataboresha maisha ya wakazi kwa kuondoa changamoto za afya ya akili, migogoro ya miundombinu na tatizo la maji safi na salama ambalo limesababisha maradhi ya mara kwa mara.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata ya Mbezi, Taliq Saad, amesema anafahamu vyema kero za wananchi, zikiwemo changamoto za maji, umeme na afya. Aliahidi pia kukuza vipaji vya vijana hususan katika michezo ya mpira wa miguu na mchezo wa masubwi ili kuwawezesha kufikia ndoto zao.