Jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ limesema kuwa limebaini uwepo wa baadhi ya watu wanaotumia mitandao mbalimbali ya Kijamii kuweka maudhui na ujumbe mbalimbali wenye kuchochea kuliingiza Jeshi hilo katika masuala ya siasa.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na uhusiano kutoka kwenye Jeshi hilo Makao makuu Kanali Bernad Masala Mlunga amewaambia waandishi wa habari leo Jumamosi Oktiba 04, 2025 kuwa baadhi ya hoja hizo zinazochapishwa mitandaoni zinatolewa na watu walio katika mazingira ya kijeshi, kujinasibisha na Jeshi pamoja na watu walioachishwa Jeshi kwa kuwa na tabia na mwenendo mbaya pamoja na kujihusisha na siasa na harakati mbalimbali.
Taarifa ya Kanali Mlunga imesisitiza kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ linaendelea kutekeleza majukumu yake Kikatiba kwa uaminifu, utii na uhodari kwa kuzingatia kiapo chao.
JWTZ wametoa taarifa hiyo siku moja mara baada ya mtu mmoja aliyejitambulisha kama Kapteni wa JWTZ John Charles Tesha, akisema yeye ni Mkufunzi wa zana za anga za kivita katika shule ya Anga (SAK) na akieleza kupitia mtandao wa Youtube kuhusu masuala mbalimbali ya siasa za Tanzania na uchaguzi Mkuu ujao, akitoa shutuma mbalimbali pia kwa baadhi ya Viongozi wal
ioko madarakani na wastaafu, familia zao na watu wao wa karibu, tuhuma ambazo hazina uthibitisho.