NA JOHN BUKUKU- NANATI MANYARA
Mbunge mstaafu wa Jimbo la Babati Mjini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pauline Gekul, amesema kuwa wananchi wa jimbo hilo hawana deni kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bali ni Rais mwenyewe anayewadai kutokana na maendeleo makubwa aliyowaletea.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Babati Mjini, Paulina alisema kuwa kabla ya uongozi wa Dkt. Samia, kulikuwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa maji, huduma duni za afya, miundombinu mibovu na ukosefu wa ajira kwa vijana.
“Kipindi cha nyuma hatukuwa na maji. Maji yalikuwa ni changamoto kubwa hapa kwetu. Lakini Mheshimiwa Rais ametutoa kwenye kiza kwa kutupatia shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji,” alisema Gekul.
Mbali na hilo, alisema kuna ujenzi mkubwa wa stendi ya kisasa ya mabasi unaoendelea, mradi unaogharimu takribani shilingi milioni 19. Pia, sekta ya afya imeboreshwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4 huku wakulima wakinufaika na ruzuku ya mbegu za mahindi.
“Mheshimiwa Rais amegusa kila sekta – afya, elimu, maji, barabara – ambazo zamani zilikuwa ni kero kubwa kwa wananchi. Sasa hivi, kila mmoja anahisi mguso wake, na ndiyo maana tunaona umati mkubwa wa watu wakijitokeza kumsikiliza,” aliongeza.
Kwa upande wa vijana, Gekul alieleza kuwa Serikali ya Rais Samia imefungua fursa nyingi kupitia ajira na mikopo ya asilimia 4 inayotolewa na halmashauri ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Pia, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kumchagua Dkt. Samia pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani kupitia CCM.
“Kama mbunge mstaafu, nimewatumikia wananchi kwa moyo mmoja. Na sasa, nawaomba wananchi wote wa Babati Mjini waunge mkono jitihada za Rais wetu kwa kumpa kura nyingi pamoja na wagombea wa chama chetu,” alisema Gekul.
Aliwaasa wanachama wa CCM kuwa wazalendo kwa kuunga mkono yeyote atakayeteuliwa kugombea nafasi mbalimbali, akibainisha kuwa tofauti za mchakato wa uteuzi hazipaswi kuleta migawanyiko ndani ya chama.
“Mimi pia napambana na nampigania Rais wetu na wagombea wote waliopitishwa na chama. Huu ni wakati wa kuonyesha mshikamano, si mgawanyiko,” alisisitiza.