NA JOHN BUKUKU- BABATI MANYARA
Babati. Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema sekta ya madini itaendelea kuwa kipaumbele cha serikali yake iwapo atapewa ridhaa ya kuunda serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku akiahidi kuendeleza wachimbaji wadogo na kupima maeneo mapya ya madini.
Akihutubia wananchi leo Jumamosi, Oktoba 4, 2025, katika Viwanja vya CCM Sabasaba Babati Mjini mkoani Manyara, Dkt. Samia alisema serikali yake itaendelea kutoa fursa kwa vijana kupitia ajira zitakazotokana na sekta ya madini, ikiwemo hatua ya kurejesha maeneo ambayo yalikuwa chini ya wawekezaji lakini hayakuendelezwa, ili yagawiwe kwa wachimbaji wadogo.
“Kipaumbele chetu ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo pamoja na kupima maeneo mapya yenye madini. Hii itapanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha wananchi na mapato ya serikali. Ndio maana maeneo yaliyokuwa mikononi mwa wawekezaji bila kufanyiwa kazi tumeyarudisha kwa wachimbaji wadogo,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, alibainisha mafanikio yaliyopatikana kwenye awamu yake ya kwanza, ikiwemo ujenzi wa kituo cha uuzaji wa pamoja wa madini ya Tanzanite Wilayani Simanjiro na kufanikisha mnada wa kwanza wa Tanzanite nchini, hatua ambazo alisema zimeongeza thamani ya madini ndani ya nchi na kuvutia wawekezaji zaidi.
Dkt. Samia alisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha sekta ya madini inabaki kuwa injini ya kukuza uchumi wa taifa, ajira na mapato ya kigeni kwa Watanzania wote.