Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amepokea wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani walioamua kujiunga na CCM kutokana na kuvutiwa na utekelezaji wa sera na maono ya Mgombea wa Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wanachama hao ni aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro kupitia ACT Wazalendo, Bw. Olekai Letion Laizer, aliyekuwa Katibu wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Simanjiro, Bw. Daniel Lucas pamoja na Bw. Abubakari Abdalah, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Babati Mjini na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kupitia chama hicho.
Wakizungumza mara baada ya kupokelewa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Stendi ya zamani ya mabasi Babati, mkoani Manyara, wameeleza kuwa hatua yao imechochewa na imani waliyo nayo kwa kazi kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea Watanzania maendeleo, kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kujenga siasa za staha na uzalendo.
Walisema tofauti na upinzani ambao mara nyingi hujikita katika siasa za kebehi, matusi na chuki, CCM chini ya uongozi wa Dkt. Samia imeonyesha mwelekeo wa maendeleo unaoweka mbele maslahi ya Taifa.