NA JOHN BUKUKU- MANYARA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana aliwahutubia wananchi wa Wilaya ya Hanang, Katesh mkoani Manyara, ambapo aliahidi kuimarisha zaidi sekta ya kilimo kwa kuwekeza kwenye zao la ngano linalolimwa kwa wingi katika maeneo hayo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Stendi ya Mabasi Katesh, Rais Dkt. Samia alisema Serikali yake imeweka mpango mahsusi wa kuliongezea thamani zao la ngano kwa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, pembejeo kwa wakati na masoko ya uhakika.
“Hanang na Manyara kwa ujumla mmebarikiwa kuwa kitovu cha zao la ngano nchini. Serikali yangu imejipanga kuliboresha zaidi zao hili ili liwe na tija kwa wakulima na kuendeleza uchumi wa taifa. Tunataka ngano ya Hanang iwe dira ya chakula na viwanda vya ndani,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa pamoja na uboreshaji wa kilimo cha ngano, Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara na masoko ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuwapatia wakulima bei bora.
Aidha, aliwahimiza wakulima kujiunga na vikundi vya ushirika ili waweze kupata mikopo nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo na taasisi nyingine za kifedha ambazo Serikali imezielekeza kutenga mikopo ya wakulima.
Wananchi wa Katesh walimshangilia kwa nguvu wakionesha matumaini makubwa kuwa uboreshaji wa zao la ngano utakuwa chachu ya maendeleo ya Wilaya ya Hanang na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.