Na Sophia Kingimali.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia chama cha CHAUMMA Khadija Mwago, ameahidi kutumia asilimia 10 ya mshahara wake wa ubunge katika kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo,
Pia,ameahidi mageuzi makubwa katika sekta za elimu, afya na ajira endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.
Akizungumza na wananchi leo octoba 3,2025 katika mkutano wa kampeni, Mwago amesema wakazi wa Mbagala wamechoshwa na miundombinu mibovu, huduma duni za afya na changamoto kubwa za elimu, hivyo akawaomba wampe nafasi ili awe kiongozi wa kusimamia maslahi yao.
“Mkinipa dhamana ya kuwa mbunge wenu, nitahakikisha vijana wanapata ajira kwa kuanzisha kituo cha ujasiriamali kitakachotoa elimu na mafunzo, sambamba na kuwaunganisha kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri. Ni haki yenu na sitakubali ibaki kwenye makaratasi,” amesema.
Bi. Mwago aliahidi pia kusimamia mikopo yenye dhamana nafuu kwa vijana walioajiliwa ili waweze kujikwamua na kujiendeleza zaidi kiuchumi.
Akigusia sekta ya elimu, amesema atahakikisha serikali inasimamia azimio la kutenga asilimia 20 ya bajeti kwa elimu na kuondoa michango ya chakula shuleni.
“Watoto wetu hawatabaki nyumbani kwa sababu ya kukosa chakula. Tutahakikisha chakula shuleni kinatolewa bure. Pia tutaongeza madarasa, madawati na kutoa motisha kwa walimu,” amesema.
Aidha, aliahidi kutenga asilimia 10 ya mshahara wake kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Mbagala.
Mgombea huyo alisema haikubaliki wananchi wa Mbagala kulazimika kulipa kati ya elfu 70 hadi laki moja ili kupata huduma za afya ya uzazi pindi wanapokwenda kujifungua.
“Nitahakikisha kila kata inakuwa na zahanati. Ni aibu kubwa kata kama Mbagala Kuu kukosa zahanati,” amesisitiza.
Bi. Mwago pia ameahidi kuwa pindi atakapopewa ridhaa atahakikisha wamachinga wa Mbagala wanapatiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara na kukomesha unyanyasaji wa ukusanyaji fedha kiholela.
Akizungumzia amani na ushirikiano amesema kuwa wananchi wa Mbagala hawatakubali kushawishiwa na watu wachache kuharibu amani ya nchi iliyopo kwa maslahi ya watu hao au kikundi.
“Amani ni msingi wa maendeleo. Sisi wananchi wa Mbagala tutapiga kura kwa amani na kuilinda nchi yetu kwani sisi tunaamini Mabadiliko yanawezekana. Twende tukairejeshe heshima ya Mbagala,” amesisitiza Mwego.