Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuunguruma leo jijini Arusha katika mkutano mkubwa wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia anatarajiwa kutilia mkazo zaidi sekta ya utalii, akibainisha mikakati ya kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania. Matarajio ni kwamba atazungumzia pia hatua za serikali katika kuboresha hifadhi za taifa, kuimarisha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, pamoja na kuvutia uwekezaji katika hoteli na huduma za kitalii ili kukuza ajira na mapato ya taifa.
Aidha, Dkt. Samia anatarajiwa kurejea mchango wa filamu ya Royal Tour ambayo imeitangaza Tanzania duniani na kuongeza idadi ya wageni, sambamba na mpango wa kuboresha Uwanja wa Ndege wa Arusha ili kuongeza uwezo wa kupokea watalii wengi zaidi kwa urahisi.
Kwa kuzingatia kuwa Arusha ni kitovu cha utalii nchini, matarajio ni kwamba Dkt. Samia ataweka wazi dhamira ya CCM kuhakikisha fursa za sekta hiyo zinawanufaisha wananchi wengi zaidi, hususan vijana na wajasiriamali wadogo.
Pamoja na kutilia mkazo sekta ya utalii, Rais Samia pia anatarajiwa kugusia maendeleo katika sekta nyingine muhimu ikiwemo elimu, afya, kilimo na ujenzi wa barabara, kama sehemu ya kuendeleza jitihada za kukuza uchumi wa wananchi.
Wananchi wa Arusha na maeneo jirani wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza, huku msisitizo mkubwa ukiwa ni matarajio ya kuifanya Tanzania iendelee kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika na duniani.