NA JOHN BUKUKU- ARUSHA
Askofu Dkt. Ole Gabriel, Katibu Mkuu wa Maridhiano na Amani, amesema kuwa Tume ya Uchaguzi imeonesha jitihada kubwa kwa kufuatilia mwenendo wa uchaguzi kwa amani na utulivu, pamoja na kuhamasisha suala la upigaji kura.
Ameyasema hayo Oktoba 2, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa Biblia inamtaja Yusufu, baba wa Yesu, alipotoka Nazareti kwenda Bethlehemu kwa ajili ya kujiandikisha, akifananisha tukio hilo na wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kupiga kura kwa amani na mshikamano.
Aidha, amebainisha kuwa siasa za vurugu na mgawanyiko hazina nafasi nchini, na kwamba viongozi wa dini hawatakubali wanasiasa wanaohubiri mipasuko ya kitaifa.
Pia, Askofu Dkt. Ole Gabriel amesema kuwa Watanzania wanapaswa kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, kisha kurejea majumbani kwao na kusubiri matokeo kwa utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Naye Bishop Dkt. Eliud Isanja wa Kanisa la Kimataifa Tanzania amesema kuwa Tanzania imejenga utamaduni wa kuishi kwa amani tangu enzi za Baba wa Taifa, na kwamba urithi huo umeendelea kudumishwa na marais wote waliopita.
Pia, amesema kuwa nchi imekuwa kimbilio la amani kwa mataifa jirani, jambo linaloonesha thamani ya amani iliyopo.
Viongozi hao wa dini wametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanalinda amani, ambayo ni msingi wa mshikamano wa kitaifa na urithi wa vizazi vijavyo.