CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kusimamia na kusisitiza mfumo wa stakabadhi kwa wakulima na kwamba chama chochote kitakachokuja na sera ya kuufuta kinataka kuleta wizi na dhuluma kwa wakulima.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 1, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alipozungumza na wana CCM Mkoa wa Mtwara akiwa katika ziara ya kuwanadi na kuwaombea kura wagombea waliosimamishwa na Chama kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka.
“Wapo watu wanapinga stakabadhi ghalani bila kujua, mimi najua, miaka ile nikiwa waziri wa kilimo mimi nilikuja hapa mkulima wa korosho alikuwa analipwa sh. 300 tena siyo kwa kipimo cha kisasa, analipwa sh. 300 kwa kitu kinaitwa kangomba, mnakajua kangomba?.
“Ni kipo ambacho ni zaidi ya kilo na wanalipwa 300, katikati yuko mtu mwingine anayenunua kwa kangomba halafu anaenda kwa mwenye pesa yeye anamuuzia sh. 500 hana mkorosho hata mmoja lakini yeye anapata sh. 200 mwenye mkorosho aliyenunua salfa analipwa 300.
“Tajiri wa kihindi anazipeleka moja kwa moja mpaka India yeye analipwa sh. 2,000 mpaka 3,000, lakini mkulima wa korosho hizo hata viatu anashindwa kununua.
Amesema sasa bei ya korosho safi Mtwara inafika hadi sh. 4,000 kutoka 300 ikiwa kazi ya CCM.
“Sasa wako wengine huko, kuna vyama vinasema mkinichagua tutafuta stakabadhi ghalani, ili urudishe wizi? Maana ukiifuta unarudisha kangomba na kangomba ni wizi mtupu unamwibia mwenye korosho zake mpaka anatembea kifudifudi, anataka salfa akipiga salfa ule mti haumpi faida hata kidogo kwa sababu ya bei ni ndogo,” ameeleza.
Amesema maendeleo ni msingi wa tatu wa Chama na kwamba kila miaka mitano kinaeleza ilani yake inakuaje “na kwa kweli ilani inayomalizika tuna rekodi safi sana kwa Mtwara.”
“Hapa Mtwara wakulima wa korosho ingawa hapa ni mjini lakini hawa ni walewale tu, wakulima wa korosho wanapata salfa bila ya malipo au siyo? Kuna chama kinajua salfa hii zaidi ya CCM? Vingine vinababaisha tu,” amesisitiza.
Aidha, amesema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030, endapo kitapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza Chama kitaisimamia serikali kujenga kongani ya viwanda kwa ajili ya kubangua korosho, “hapana kuuza korosho na magamba.”