Mkuu wa wilaya ya Kalambo Dkt Lazaro Komba kushoto wakati akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji katika kijiji cha Lyapona.
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Mwenge wa Uhuru umezindua rasmi mradi wa maji wa kijiji cha Lyapona katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mradi huo umetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia program ya visima 900.
Mradi wa kisima cha Lyapona umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 72 na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi wapatao 3,239 katika kijiji cha Lyapona A na B na vijiji jirani ikiwa Lengo kuu ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, jambo linaloendana na dira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, 2025 Ismail Ali Ussi, amepongeza RUWASA kwa usimamizi na utekelezaji bora wa mradi huo.
Amesisitiza kuwa mradi wa Lyapona ni kielelezo cha dhahiri cha jitihada za Serikali kuondoa kero ya maji vijijini na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
“Miradi ya aina hii inaleta suluhisho la kudumu kwa wananchi na ni matunda ya mshikamano kati ya Serikali na wadau katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi,” Ussi amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Sumbawanga, Mhandisi Bahati Haule amesema RUWASA itaendelea kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango bora vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.
“Tuna dhamira ya dhati kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma ya majisafi na salama.
RUWASA itaendelea kusimamia miradi yote kwa ufanisi ili kufikia lengo la serikali la kufikisha maji vijijini kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025,” Mhandisi bahati amesisitiza.
Kwa upande wao wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mradi wa maji kupitia program ya visima 900 wameishukuru serikali kwa kufikisha huduma hiyo muhimu katika makazi yao na kurahisisha upatikanaji wa huduma majumbani.
Uzinduzi wa Mradi wa Maji Lyapona ni sehemu ya shughuli za Mwenge wa Uhuru 2025, unaolenga kufuatilia na kuzindua miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo maji, afya, elimu na miundombinu.